Pablo, Kaze nao waichambua dabi

02May 2022
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Pablo, Kaze nao waichambua dabi

MAKOCHA waliobeba dhamana ya kuziongoza timu zao kwenye mechi ya 'dabi' ya watani wa jadi, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco na Mwalimu Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, kila mmoja ametoa tathimini yake baada ya timu hizo kutoka suluhu katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa,

Akizungumza baada ya mechi hiyo kumalizika, Pablo alisema hawajafurahishwa na sare ya bila kufungana waliyopata dhidi ya Yanga kwa kuwa lengo lilikuwa kupata pointi zote tatu ambazo zingewafanya kuwasogelea zaidi wapinzani wao hao, lakini matokeo hayo yameipa nafasi Yanga kuwa karibu na ubingwa, ingawa hawajakata tamaa hadi mwisho wa msimu.

Alisema mchezo ulikuwa mzuri uliotawaliwa na mbinu ingawa washambuliaji na nyota wake walipaswa kutumia vizuri nafasi walizotengeneza.

"Sijafurahishwa na matokeo ya sare, tuliingia kwa nia ya kutafuta ushindi kwa kuwa tunahitaji kupunguza tofauti iliyopo na bado tunahitaji kutetea ubingwa wetu," alisema Pablo.

Kwa upande wa Kaze, alisema kipindi cha kwanza hakikuwa kizuri kwao licha ya kutengeneza nafasi na kushindwa kuzitumia kwa sababu ya wachezaji wao kutofanya maamuzi sahihi huku dakika 20 za mwisho walifanya makosa na kuwafanya Simba wamiliki zaidi mpira.

“Tulifanikiwa kuziba njia zote za Simba hasa kutoruhusu beki zao kupanda na kupeleka mashambulizi, pia hata sisi hatukuwa vizuri katika kumalizia licha ya kufika ndani ya 18,” alisema Kaze.