Mara ya mwisho Yanga kupata ushindi ilikuwa ni dhidi ya Zalan FC kutoka Sudan Kusini, katika mechi iliyochezwa Septemba 17, mwaka jana ikiwa ni hatua za awali za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema wamewaeleza wachezaji wao wanachama na mashabiki wanahitaji kupata ushindi katika mechi hiyo itakayochezwa Jumapili.
Kamwe alisema kuwapo kwa wachezaji raia wa DRC katika kikosi chao ni faida kubwa watapowakaribisha TP Mazembe katika mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika.
"Hili la Yanga kutofanya vyema kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, hiyo ni sahihi kwa sababu takwimu zinaonyesha hivyo na wala si jambo la kubishania wala mawazo ya mtu. Ni kweli hatuna matokeo mazuri kwenye uwanja huo, siwezi kusimama hapa nikaanza kukanusha, na moja kati ya vitu ambavyo tumezungumza na wachezaji hilo lilikuwapo.
Hatukushinda nyumbani, tukafanya hamasa nyingine kubwa kuelekea kwenye mechi yetu dhidi ya Club Africain uliopigwa nyumbani, mwisho wa siku matokeo yake yalikuwa suluhu," alisema Kamwe.
Aliongeza wamewakumbusha wachezaji kupambana na kuhakikisha wanasaka matokeo mazuri kwa ajili ya kuwasahaulisha machungu wanachama na mashabiki wao.
"Hatuwezi kila siku tunafanya hamasa mitaani kukusanya watu, halafu watu wakija timu haipati matokeo mazuri, kwa hiyo safari hii ni jukumu la kuhakikisha tunavunja mwiko wa kutoshinda kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa," alisema Kamwe.
Alisema pamoja na ubora wa TP Mazembe, lakini wao wana wachezaji ambao wameshazoea kucheza na timu hiyo walipokuwa na AS Vita ambao ni Fiston Mayele, Djuma Shaaban, Yannick Bangala, Jesus Moloko na Tuisila Kisinda.
"Wachezaji wetu hawa walikuwa AS Vita Club na haikuwa mechi ya kawaida, walikuwa wakicheza na TP Mazembe mechi ya 'dabi', nyingine Kinshasa, halafu tena wanakwenda kucheza Lubumbashi, kwa hiyo wengi hawana ugeni sana kucheza dhidi ya timu hiyo. Hii haitotusaidia hapa tu, hata mechi ya ugenini," Kamwe aliongeza.










