Kabla ya kutwaa taji hilo linalowapa tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika, kikosi hicho cha Jangwani kilitwaa taji la Ligi Kuu Bara kabla ya kumalizika msimu na kunyakua Sh. milioni 81, hivyo kufunga mahesabu ya mkwanja wakiwa na Sh. milioni 131.
Iliwachukua Yanga dakika 9 tangu filimbi ya kuanza mchezo kupulizwa kufunga bao la kuongoza kupitia kwa mshambuliaji Amiss Tambwe.
Tambwe alifunga bao hilo kwa kichwa akiichangamkia fasta krosi ndefu ya beki Abdu Juma, ambayo pia ilikuwa ikiwaniwa kuchezwa kipa wa Azam FC, Aishi Manula.
Dakika mbili ndani ya kipindi cha pili, Tambwe alizigusa tena nyavu za Azam kwa kufunga bao la pili kwa shuti akimaliza krosi ya Msuva.
Azam walijibu mapigo na kufunga bao pekee kwenye kupitia kwa Didier Kavumbagu aliyemalizia krosi ya Ramadhan Singano. Kavumbagu aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya John Bocco.
Mabingwa Yanga walikamilisha furaha ya ushindi kwa kufunga bao 'tamu' la tatu likiwekwa kimiani na Deus Kaseke aliyemalizia kazi nzuri ya Msuva, aliyetengenezewa pande na Thabani Kamusoko.
Katika mechi hiyo, Yanga ilitawala sehemu kubwa na ingeweza kuibuka na ushindi mkubwa kama washambuliaji wake wangetumia vizuri nafasi nyingi za kufunga walizopata.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema matokeo hayo mazuri kwa timu yake yalitokana na kujituma kwa ajili ya kufikia malengo ya kutwaa mataji mawili msimu huu.
Beki wa Yanga, Juma Abdul alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mashindano, huku Aishi Manula akitwaa tuzo ya kipa bora na Atupele Green mfungaji bora.
Yanga: Deogratius Munishi 'Dida', Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Vincent Bossou, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Haruna Niyonzima, Donald Tambwe na Deus Kaseke.
Azam FC:
Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Aggrey Morris, Abdallah Kheri, Jean Mugiraneza ' Migi' ,Ramadhan Singano 'Messi',Mudathir Yahya, Himis Mao, Farid Mussa na John Bocco.










