Nabi aliuagiza uongozi wa klabu hiyo kumtafutia mikanda ya video ya hivi karibuni ya wapinzani hao na tayari amekabidhiwa.
Yanga wataanzia nyumbani mchezo wa fainali Mei 28 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam kabla ya kurudiana nao Juni 3, mwaka huu nchini Algeria.
Akizungumza na Nipashe jana, Nabi alisema tayari kwa kupitia video alizopewa ameona ubora na udhaifu wa wapinzani wao hao na kwa sasa anafanyia kazi mbinu zitakazomwezesha kupata ushindi kwenye mchezo wa kwanza nyumbani.
Nabi alisema michezo hiyo miwili ya fainali ni michezo ya matokeo zaidi hivyo anaandaa mbinu itakayowapa matokeo mazuri kwenye michezo yote ili kuweza kutwaa ubingwa wa Afria kwa mara ya kwanza.
“Mechi itakuwa ya ushindani mkubwa nalihitaji kuwafuatilia wapinzani wetu jinsi wanavyocheza wanapokuwa ugenini na nyumbani, nafurahi nimepata mikanda yao na bado tunaendelea kuifanyia kazi ingawa nimeona ubora na hata udhahifu wa wapinzani wetu, mechi hizi mbili ni mechi za matokeo zaidi,” alisema Nabi.
Alisema moja ya kazi aliyoifanya ni kuwabaini wachezaji bora wa USM Alger na kuwapa mbinu wachezaji wake namna ya kukabiliana nao.
"Niwapongeze wachezaji wangu wamepambana na kufanikiwa kufika fainali ya michuano hii ya CAF, kazi iliyobaki kwetu ni kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye hatua hii, kuna mbinu ambazo tunazifanyia kazi na kuwapa wachezaji wetu, tunaamini tutafanya vizuri,” alisema Nabi.
Alisema pia anashukuru viongozi wa Yanga kwa kushirikiana naye bega kwa bega kuanzia mwanzo wa msimu kwa kufanya usajili mzuri na kuhakikisha wanapata mahitaji yote.
Nabi anasema tayari amewaambia wachezaji wake kuwa ni lazima wamalize kazi kwenye mchezo wao wa nyumbani ili kujiweka katika mazingira mazuri kuelekea kwenye mchezo wa marudiano.
Alisema wamegundua mbinu wanazozitumia wapinzani wao kwenye michezo ya ugenini na ile wanayotumia kwenye michezo wanayokuwa nyumbani.
“Jambo kubwa ambalo kama benchi la ufundi tunalifanyia kazi kwa umuhimu mkubwa ni kutafuta namna ya kuhakikisha tunamaliza kazi kwenye mchezo wetu wa nyumbani, tupate ushindi mzuri ambao utatupa picha ya nini cha kufanya kuelekea kwenye mchezo wa marudiano,” alisema Nabi.
Yanga inahitaji ushindi mzuri kwenye mchezo wa kwanza hapa nyumbani kabla ya kuelekea jijini Alger nchini Algeria kwa ajili ya mchezo wa marudiano.










