Mwakinyo, Okwiri ulingoni Septemba 29

08Sep 2023
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Mwakinyo, Okwiri ulingoni Septemba 29

BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo, anatarajia kupanda ulingoni kupigana na Mkenya, Rayton Okwiri, katika pambano la kuwania mkanda wa ubingwa wa IBA.

BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo.

Pambano hilo linatarajia kufanyika Septemba 29, mwaka huu kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Akizungumza na Nipashe Digital, promota wa pambano hilo, Ali Mndeme, alisema tayari makubaliano ya kuandaa pambano hilo kati ya IBA na Mwakinyo yamefikia katika hatua nzuri.

Mndeme alisema wanatarajia pambano hilo litakuwa na ushindani kutokana na ubora wa mabondia wanaokutana.

“Litakuwa pambano la kuwania mkanda wa kimataifa, tumejipanga vizuri safari hii moto utawaka, kwa sababu mbali na pambano hilo ambalo litakuwa kubwa, pia tutakuwa na mapambano ya utangulizi makali,” alisema Mndeme.

Aliongeza Mwakinyo anaendelea vyema na mazoezi ya kujiandaa na pambano hilo na amejipanga kupeperusha vizuri bendera ya Tanzania.

“Kila kitu kinakwenda vizuri, tunatarajia kuwa na pambano lenye hadhi ya kimataifa, kila bondia atakayepanda ulingoni ataonyesha ubora wake, tunawaomba wadau wa mchezo wa ngumi waje kupata burudani,’ aliongeza promota huyo.