Morocco aanika mbinu kuishika Mashujaa FC

24Aug 2023
Adam Fungamwango
Nipashe
Morocco aanika mbinu kuishika Mashujaa FC

KOCHA Mkuu wa Geita Gold FC,  Hemed Suleiman 'Morocco', amesema suluhu waliyoipata kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma dhidi ya timu machachari ya Mashujaa FC ni kutokana na kuwazuia kucheza staili yao ya kupiga mipira mirefu ya juu kwani nguvu yao ndipo ilipo.

 

Akizungumza juzi mara baada ya kumalizika mechi hiyo ya raundi ya pili ya Ligi Kuu, Morocco alisema kilichoisaidia timu yake kuondoka salama Kigoma ni kuwazuia Mashujaa kucheza soka lao walilozoea la kutumia nguvu nyingi na kupiga mipira mirefu.

"Nashukuru Mungu pamoja na kuwapongeza wachezaji wangu kwa sababu wamecheza kwa bidii sana, wamecheza soka la kasi ambalo nilitegemea kuwa litaoneshwa leo (juzi) kwenye uwanja huu, kwa sababu wapinzani wetu niliwasoma wanacheza soka la nguvu pamoja na kupiga mipira mirefu ya juu, hivyo niliwatengeneza vijana wangu wawe wanakimbia sana, kuziba mianya na kuzuia mipira yote mirefu isiwafikie walengwa," alisema Morocco.

Pamoja na hayo, Morocco alisema wao walijaribu kuweka mpira chini na kadri muda ulivyozidi kwenda mbele ndivyo wachezaji wake walivyozidi kuumiliki mpira, jambo ambalo linamfanya kuona mwanga mzuri kwenye kikosi chake kuelekea mechi zijazo.

Mohamed Abdallah 'Bares', Kocha Mkuu wa Mashujaa, yeye alisema safu yake ya ushambuliaji kwa mechi ya juzi haikuwa makini kwani walitengeneza nafasi ambazo hazikutumiwa vema.

"Huu ndiyo mpira, tumepata suluhu, hatukutumia nafasi tulizozipata, safu ya ushambuliaji haikuwa makini, lakini tutakwenda kulifanyia kazi mazoezini," alisema.

Suluhu hiyo inazifanya timu hizo kufikisha pointi nne kila moja, huku ikiwa ni sare ya kwanza kwa Mashujaa ikiwa uwanja wake wa nyumbani baada ya kushinda mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar mechi ya awali, Geita Gold yenyewe iliidungua Ihefu FC bao 1-0 ugenini.