Kipigo hicho pia kilikuwa cha kwanza kwa kocha wa muda, Jackson Mayanja baada ya kushinda mechi sita mfululizo tangu arithi mikoba ya Mwingereza Dylan Kerr aliyetumiliwa Januari 10 baada ya timu hiyo ya Msimbazi kufungwa bao 1-0 na Mtibwa na kuvuliwa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.
Mabao mawili ya washambuliaji Donald Ngoma na Amissi Tambwe yalitosha kupeleka 'kilio' kwa Wanamsimbazi ambao walicheza dakika 65 za mwisho wakiwa pungufu kwa mchezaji mmoja baada ya Abdi Banda kuonyeshwa kadi mbili za njano ndani ya dakika tatu (22 na 25).
Kwa matokeo hayo, Yanga waliwang'oa wapinzani wao wa jadi kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo wakifikisha pointi 46 baada ya mechi 19, pointi moja mbele ya Simba walioporomoka hadi nafasi ya tatu, huku Azam FC wakipanda hadi nafasi ya pili.
Ushindi huo pia umeifanya Yanga kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kushinda mechi zote mbili dhidi ya Simba msimu huu na timu pekee iliyoshinda dhidi ya Wanamsimbazi kwenye Uwanja wa Taifa msimu huu.
Straika wa kimataifa kutoka Zimbabwe, Ngoma aliifungia Yanga goli lililodumu kipindi chote cha kwanza akitumia makosa ya beki wa pembeni kulia, Hassan Kessy kwa kuunasa mpira uliorudishwa kizembe kwa kipa Vincent Angban na mchezaji huyo wa zamani Mtibwa Sugar.
Kabla ya kufunga goli lake la 11 Ligi Kuu Bara msimu huu, mshambuliaji huyo ambaye amekuwa msaada mkubwa kwa kikosi cha Wanajangwani tangu asajiliwe msimu huu, alimlamba chenga kipa huyo wa kimataifa kutoka Ivory Coast kabla ya kupiga shuti 'mtoto' kwa mguu wa kulia ndani ya sita.
Goli hilo la 34 Yanga kufunga kwenye Uwanja wa Taifa msimu huu, lilionekana kuchagizwa na kujisahau kwa safu ya ulinzi ya Simba, ambayo ilimkosa Banda aliyelimwa kadi nyekundu na refa Jonesia Rukyaa kutokana na kumchezea rafu Ngoma dakika za 22 na 25.
Dakika 18 kabla ya mechi hiyo kumalizika, Mfungaji Bora wa ligi hiyo msimu wa 2013/14, Tambwe, alitupia goli lake la 15 msimu huu na la pili kwa Yanga jana akimalizia kwa shuti kali la mguu wa kulia mpira wa krosi ya wingi ya kushoto iliyopigwa na mtokeo benchini Geofrey Mwashiuya.
Baada ya kutupia goli hilo lililomfanya awe nyuma kwa goli moja dhidi ya kinara Hamis Kiiza wa Simba, Mrundi huyo aliweka mikono yake chini na kubusu ardhi ya ndani ya sita ya lango la Simba kaskazini mwa Uwanja wa Taifa.
Tambwe pia alifunga goli la kwanza la Yanga walipoifumua Simba mabao 2-0 kwenye uwanja huo katika mechi yao ya duru la kwanza. Goli la pili lilifungwa na mshambuliaji Malimi Busungu, ambaye jana hakucheza.
Simba ndiyo walioanza kwa kuutawala kwa kiasi kikubwa mchezo huo kabla mambo hayajawaendea kombo kutokana na kucheza pungufu.
Katika robo saa ya mchezo, shuti la ndani ya boksi lililopigwa na Ibrahim Ajibu aliyeunganisha mpira wa kosa ya Hassan Kessy iliyobabatizwa kwa kichwa na Hamis Kiiza, lilifutwa vyema na beki Vincent Bossou na kuwanyima Simba goli la kuongoza.
Kiungo mkabaji Jonas Mkude pia alikaribia kufunga katika dakika ya 18 lakini shuti lake la mguu wa kushoto ndani ya boksi liligonga nguzo baada ya kutokea kizaazaa kwenye lango la Yanga.
Kukosekana kwa umakini katika umaliziaji uliinyima Simba uongozi wa mechi katika dakikka 20 za mwanzo, huku washambuliaji wao pia wakishindwa kuzitumia vyema kona saba ambazo timu hiyo ya Msimbazi ilipata kipindi chote cha kwanza. Yanga hawakupata kona hata moja kipindi kipindi chote cha kwanza.
Nafasi nzuri zaidi waliyoipata Simba kipindi cha pili ilikuwa katika dakika ya 64 mshambuliaji wa zamani wa Coastal Union na FC Lupopo, Dany Lyanga alipowachambua vizuri mabeki wa Yanga kabla ya kumtengea mpira Said Ndemla nje kidogo mwa boski lakini shuti la mguu wa kulia wa kiungo huyo halikulenga lango la Yanga.
MATUKIO/ MBWEMBWE
Kabla ya kuanza kwa mechi hiyo ya pili ya watani wa jadi msimu huu, kulikuwa na mbwembwe za viongozi na wanachama wa klabu hizo, Januari Makamba na Mwingulu Nchemba wakiwaongoza mashabiki wa Yanga.
Mashabiki kadhaa wa timu zote (wanne wa Yanga) walianguka na kupoteza fahamu uwanjani wakati wa mechi hiyo ya raundi ya 20.
Matokeo mengine
Stand United 1 - 1 JKT Ruvu
Mbeya City 0 - 3 Azam FC
Toto Africans 1 - 1 Kagera Sugar
Mwadui FC 0 - 0 Prisons
Vikosi vilikuwa:
Yanga: Ally Mustafa, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Mbuyu Twite, Vincent Bossou, Pato Ngonyani, Deus Kaseke/ Geofrey Mwashiuya (dk 64), Thaban Kamusoko, Donaldo Ngoma, Amissi Tambwe na Haruna Niyonzima/ Simon Msuva (dk 52).
Simba: Vincent Angban, Hassan Kessy, Mohamed Hussein, Abdi Banda, Juuko Murshid, Justicwe Majabvi, Said Ndemla, Jonas Mkude, Hamis Kiiza/ Danny Lyanga (dk 60), Ibrahim Ajibu/ Brain Majwega (dk 80) na Mwinyi Kazimoto/ Novalt Lufunga (dk 46).
Imeandikwa na Faustine Feliciane, Renatha Msungu, Adam Fungamwango, Sanula Athanas na Somoe Ng'itu (Dar)










