Nyota mwingine anayetajwa kuwindwa na Simba ni kiungo Brazil Bruno Gomes, ambaye amekuwa na kiwango kizuri katika msimu wake wa kwanza aliowatumikia Singida Big Stars ya mkoani Singida.
Miquissone aliondoka Simba na kujiunga na Waarabu hao baada ya kuonyesha kiwango cha juu, lakini 'Mmakonde' huyo ameshindwa kuwa na wakati mzuri huko Misri.
Akizungumza na Nipashe, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema mpango huo upo na wanachosubiri ni kufahamu kiasi gani cha fedha Al Ahly itahitaji ili kutoa baraka za mchezaji huyo kurejea Tanzania.
Ahmed alisema mchakato huo hauna mashaka kwa sababu iwapo Al Ahly watataka kumuuza ni lazima wawasiliane na Simba kama walivyokubaliana wakati wanamuuza mwaka 2021.
" Luis ni mchezaji wa Al Ahly, lazima mashabiki wa Simba waelewe ana mkataba wa klabu hiyo, na makubaliano ya Al Ahly na sisi tuliyoingia ni endapo wakitaka kumuuza wanapaswa kwanza kuiambia Simba, kwa hiyo tutawasikiliza kama wanamuuza watatuambia, watatutajia na bei.
Mambo yakiwa mazuri tutafanya biashara, yote kwa yote mchezaji huyu akitua Msimbazi kila mmoja anajua balaa lake, kuhusu pesa wala hatuna matatizo kabisa msimu huu tumedhamiria, tutamsajili yoyote ambaye tutamhitaji," alisema Ahmed.
Nyota huyo juzi alionekana katika video akifanya mazoezi binafsi akiwa na jezi namba 17 ya Timu ya Taifa ya Zambia (Chipolopolo), ambayo huvaliwa kiungo wa Simba, Clatous Chama.
Mashabiki wa klabu hiyo wanatafsiri hizo ni dalili kuonyesha huenda mchezahu huyo anajiandaa kurejea tena katika klabu yake ya zamani na kufanya makubwa kama ilivyokuwa awali.
Chama alimjibu kwenye akaunti yake instagram kwa maneno ya mzaha, akiandika "piga ugali mkubwa."
Tangu ajiunge na Al Ahly, mchezaji huyo amekuwa si sehemu ya kikosi cha kwanza na amekuwa akatolewa kwa mkopo kwenye klabu ya Abha FC ya Saudi Arabia.
Awali, mchezaji huyo alijiunga na Simba 2020 akitokea UD Songo ya Msumbiji, alipokuwa akiichezea kwa mkopo kutoka klabu mama ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, lakini ilimpiga bei 2021 kwenye klabu hiyo kubwa Afrika, akiwa pamoja na Chama ambaye aliuzwa RS Berkane, lakini kwa sasa amerejea tena kwenye klabu yake ya zamani.
Wakati huo huo, taarifa zilizopatikana Dar es Salaam zinasema Bruno amekuwa katika mipango ya Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliviera 'Robertinho'.
Chanzo chetu kinasema mabosi wake wa Singida Big Stars ambayo msimu ujao itashiriki mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika wamekataa kusema chochote kuhusiana na tetesi za kuondoka kwa mchezaji wao.
"Ni mapema kusema lolote, suala la usajili linahitaji baraka ya klabu nzima, kwa sasa hakuna uamuzi wowote uliofanyika, siwezi kusema Bruno anakwenda wapo msimu ujao," kilisema chanzo chetu.
Mapema baada ya kuonyesha kiwango kizuri, kiungo huyo alionekana kuwa na dalili za kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga.










