Mbappe rasmi sokoni

15Jun 2023
Nipashe
Mbappe rasmi sokoni
  • Mtazamo mpya ungekuwa kwa vijana na alitarajiwa kuwa kiini cha...

KLABU ya Paris St-Germain iko tayari kumuuza Kylian Mbappe msimu huu wa joto kwa hofu ya kumpoteza kama mchezaji huru mara mkataba wake utakapomalizika mwakani, baada ya kuiambia klabu hiyo ya Ufaransa kuwa hataongeza mkataba wake.

Kylian Mbappe.

Mkataba wa sasa wa mchezaji huyo wa Ufaransa unamalizika mwishoni mwa msimu ujao, kukiwa na chaguo la kuongeza mwaka mwingine.

Huku PSG wakiwa hawataki Mbappe aondoke kama mchezaji huru baada ya msimu ujao, duru zilisema mwenyekiti wa klabu hiyo, Nasser Al Khelaifi sasa yuko wazi kumruhusu mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 kuondoka jijini Paris.

Vyanzo vya ESPN viliongeza kuwa PSG itataka ada itakayofikia euro milioni 150 ili kumwachia. Mwaka jana, PSG ilikataa dau la euro milioni 180 kutoka kwa Real Madrid, ambao walikuwa wanamtaka Mbappe tangu akiwa na umri wa miaka 11.

Mshambuliaji huyo huenda akahusishwa tena na kuhamia Madrid, hasa baada ya Karim Benzema kuwaacha wababe hao wa LaLiga na kujiunga na timu ya Al-Ittihad ya Saudi Arabia.

Madrid tayari wamekubali kumnunua kiungo wa kati wa England, Jude Bellingham na uwezekano wa kumpata Mbappe utakuwa kauli ya dhamira kuu baada ya kuachia mataji yao ya LaLiga na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Mbappe alikuwa amekataa kuzungumzia mustakabali wake na PSG kufuatia kutolewa kwenye hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Bayern Munich, Machi.

PSG, ambayo inamilikiwa na Qatar Sports Investments, tayari imemuona Lionel Messi akiondoka bila malipo, huku nyota huyo wa Argentina akihamia timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani, MLS, Inter Miami.

Pia kuna sintofahamu kuhusu mustakabali wa nyota mwingine wa PSG raia wa Brazil, Neymar.

Lakini uwezekano wa kuondoka kwa Mbappe mwenye umri wa miaka 24 itakuwa hasara kubwa zaidi kwa PSG, ikizingatiwa kwamba yeye ni nyota anayechukuliwa kuwa mmoja wa wachezaji wachache wenye uwezo wa kuchukua mikoba ya Messi na Cristiano Ronaldo kama nyota mkubwa zaidi wa mchezo huo duniani.

Mbappe alikuwa na hadi Julai 31 kuanzisha mazungumzo ya kuongeza mkataba wa mwaka mmoja.

Amekuwa katika klabu hiyo tangu mwaka 2017 baada ya kusajiliwa kutoka AS Monaco kwa uhamisho wa thamani ya dola milioni 190.

PSG walikuwa wakipanga mabadiliko ya mkakati baada ya uhamisho wa nyota hao wakubwa kushindwa kuleta mafanikio Ulaya.

Mtazamo mpya ungekuwa kwa vijana na Mbappe alitarajiwa kuwa kiini cha mabadiliko hayo na ilitarajiwa angesaini mkataba wa muda mrefu zaidi.

Mbappe ameshinda mataji matano ya ligi ya Ufaransa akiwa na PSG na alikuwa mshindi wa Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa mwaka 2018.

Ana mabao 38 katika mechi 68 alizoichezea Ufaransa, ikiwa ni pamoja na mabao matatu kwa mpigo katika fainali ya mwaka jana nchini Qatar, Ufaransa ilipofungwa na Argentina kwa mikwaju ya penalti.

Mbappe alimaliza kama mfungaji bora wa Ligue 1 katika kila misimu mitano iliyopita.

PSG ilimaliza msimu wa 2022-23 kwa kutwaa taji la Ligue 1 pekee baada ya kushindwa tena kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.