Mayele aanza kuigusa Simba

13Mar 2023
Saada Akida
Nipashe
Mayele aanza kuigusa Simba
  • Ni wakati wakisaka pointi 18 za kufunga msimu wa Ligi Kuu, akata tamaa kuishika rekodi ya...

WAKATI miamba ya soka nchini, Simba na Yanga kila moja ikibakiza mechi moja kabla ya kukutana Aprili 16, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, mshambuliaji wa vinara hao wa Ligi Kuu Bara, Fiston Mayele, ametangaza hali ya hatari ya kucheka na nyavu.

Fiston Mayele,

Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi hiyo, Yanga itaikaribisha Kagera Sugar Aprili 7, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kesho yake Simba itakuwa ugenini mkoani Mbeya kuvaana na Ihefu FC na baada ya michezo hiyo, mechi itakayofuata itakuwa Aprili 16, mwaka huu, kwa miamba hiyo kuvaana.

Hata hivyo, kuelekea michezo sita ya ligi hiyo iliyobaki kwa miamba hiyo kabla ya ligi kufikia ukingoni, Mayele amewatangazia wapinzani wao kuwa malengo yao ni kutaka kukusanya pointi 18 katika mechi hizo zilizosalia.

Kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Geita Gold FC uliopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam, Yanga watakuwa na michezo sita iliyosalia ya ligi hiyo ikiwamo dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa Chamazi na Simba Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mechi zingine dhidi ya Singida Big Stars utakaopigwa katika Uwanja wa Liti mjini Singida, Dodoma Jiji FC utakaopigwa Dimba la Azam Complex na michezo miwili itakayopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons, ambayo yote Mayele amepania kuipa timu yake alama tatu kila mmoja.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mayele alisema mikakati yao ni kushinda mechi zote zilizopo mbele yao ili kuendelea na rekodi yao ya kutopoteza mechi tangu Novemba 29, mwaka jana walipokubali kipigo cha mabao 2-1 ugenini dhidi ya Ihefu FC.

Alisema wapinzani wao watakaokutana nao wajiandae vizuri kwa sababu mikakati yao ni kuendeleza rekodi ya kutopoteza pointi yoyote katika michezo sita iliyosalia ya ligi hiyo.

“Ligi imekuwa ya ushindani na sasa tunaelekea ukingoni mwa msimu, wapinzani wetu wajiandae vizuri kwani dhamira yetu ni kushinda mechi zote sita na kuvuna pointi 18, suala la kuwania tuzo ya ufungaji bora bado lipo palepale.

"Kwa sasa kipaumbele changu ni kuona Yanga inapata matokeo mazuri katika michezo sita iliyosalia kwa kukusanya pointi zote 18 ili kutetea taji la ubingwa baada ya hapo ndio mambo ya ufungaji bora yanafuata,” alisema Mayele.

Alisema kwake binafsi muhimu sana ni malengo ya timu kwa sababu wanahitaji kutwaa ubingwa kwa mara nyingine msimu huu.

Mayele alisema mshambuliaji yeyote lazima awe na malengo binafsi na kwamba kwa sasa michezo iliyosalia hawezi kufunga mabao mengine 11 ili kufikia rekodi ya nyota wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein 'Mmachinga' aliyoiwekwa 1997 ya kufunga mabao 26 katika mechi 24 tu za ligi hiyo.

Hadi sasa Mayele ameshacheka na nyavu mara 15, hivyo kwa mechi zilizosalia inaonekana pia itakuwa vigumu kufikia hata rekodi ya Abdalah Juma (Mtibwa) ya mabao 25 mwaka 2005, Meddie Kagere (Simba) mabao 23 msimu wa 2018/19, Amissi Tabwe (Yanga) mabao 21 msimu wa 2015/16 na  Emanuel Okwi (Simba) mabao 20 msimu wa 2017/18.