Mauti ilivyomkuta Bayo

12Apr 2023
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Mauti ilivyomkuta Bayo

ALIYEKUWA Makamu wa Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), John Bayo, amefariki dunia.

John Bayo.

Katibu wa Kamisheni ya Wanariadha nchini, Andrew Robbi, akizungumza na Nipashe jana, alisema Bayo alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya figo kwa muda mrefu na kumsababishia kutolewa figo moja.

Alisema alianza kusumbuliwa na maradhi hayo tangu Desemba mwaka jana kwa kutibiwa Hospital ya Ocean Road, Dar es Salaam kabla ya Ijumaa iliyopita kwenda Arusha.

"Alikuja Arusha huku akiendelea kujiuguza, lakini jana (juzi) alijisikia vibaya na hali ikazidi kubadilika na kupelekwa katika HospitalI ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu na hapo ndipo mauti ilipomkuta," alisema Robbi.

Aidha, taarifa iliyotolewa jana mchana na RT, ilieleza kuwa Bayo alifariki dunia jana jijini Arusha.

Aidha, taarifa hiyo imemwelezea Bayo kuwa ni kati ya mawakala wa kwanza kupeleka wanariadha barani Ulaya kuanzia miaka ya 1980 na ameendelea kuwa nguzo kuu katika uongozi wa mchezo huo hadi mwisho wa uhai wake.

Bayo aliliongoza shirikisho hilo mwaka 2021 akiwa Makamu wa Rais kwa muda wa miezi sita kutoka Januari, hadi alipojiuzulu Agosti, akiwa chini ya Rais wa Shirikisho hilo, Silas Isangi.

Marehemu alikuwa ni mmoja kati ya wataalam wawili wenye kozi ya upimaji wa njia za mbio na kutambulika na Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Riadha (IAAF) akiwa na Daraja B.

Taarifa ya Shirikisho hilo imesema kuwa mipango ya mazishi na  mengineyo itatolewa baadaye.

 

Imeandikwa na Adam Fungamwango na Saada Akida