Majimaji wakana vurugu Mbeya City

23Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Majimaji wakana vurugu Mbeya City

UONGOZI wa klabu ya Majimaji ya Songea, mkoani Ruvuma, umedai kushangazwa na kusikitishwa na kauli zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa klabu ya Mbeya City ya jijini Mbeya zilizodai kuwapo kwa vurugu wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Bara kati ya timu hizo kwenye Uwanja wa Majimaji Jumamosi.

klabu ya Majimaji ya Songea.

Katika tuhuma walizotoa, viongozi wa Mbeya City wamedai kuwa vurugu hizo zilisababisha mashabiki wa timu ya Majimaji kuvunja kioo cha gari la timu hiyo ya Mbeya.

Akizungumzia tuhuma hizo zilizonukuliwa na vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Majimaji, Humphrey Milanz, alisema madai hayo hayana ukweli wowote na hakuna tukio la namna hiyo lililotokea ndani ya uwanja huo wa Majimaji zaidi ya mashabiki wa timu ya Mbeya City kuwarushia chupa za maji wachezaji wa timu ya Majimaji wakati wakishangilia goli la pili.

Alisema muda wote wa mchezo huo, askari wa jeshi la Polisi na kampuni binafsi za ulinzi walikuwapo ndani ya uwanja kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na hakuna gari lolote lililoingia uwanjani ambalo lilishambuliwa na hata kuvunjwa kioo kama ilivyodaiwa na baadhi ya viongozi wa Mbeya City.

Milanzi alisema kauli hizo zinalenga kuharibu uhusiano mwema uliopo kati ya timu hizo mbili tangu zikiwa katika mashindano ya soka ligi daraja ambako timu ya Mbeya City ilifanikiwa kuingia ligi kuu ikicheza mchezo wake wa mwisho dhidi ya Majimaji na hakujawahi kuwapo kwa tofauti zozote kati ya timu hizo.

Aidha, aliongeza kuwa zipo taratibu zinazosimamia soka nchini zinazopaswa kufuatwa na kuchukuliwa kama vitendo vya vurugu vinafanywa na mashabiki wa timu mojawapo na kusababisha uharibifu wa mali ikiwamo kutoa taarifa kwenye mamlaka husika.