Magese aiangukia Serikali vifaa tiba

31Mar 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
Magese aiangukia Serikali vifaa tiba

MISS Tanzania (2001) na mwanamitindo wa kimataifa, Millen Happiness Magese, ameiomba serikali kuwekeza katika vifaa vya tiba ya ugonjwa wa Endometriosis (ugumba) ili kuepusha wasichana wa Tanzania kukumba na ugonja huo.

Millen Happiness Magese.

Akizungumza jana katika semina maalum iliyoshirikisha zaidi ya wanafunzi 400 wa kike wa Shule za Sekondari mbalimbali, Dar es Salaam, Millen alisema kama serikali itaongeza nguvu kupata vifaa hivyo, itasaidia kupunguza tatizo hilo linalowakabili mamilioni ya wanawake duniani.

Millen alisema serikali pia ikiandaa programu za mafunzo, itasaidia kutoa elimu kuhusiana na ugonjwa huo ambao huchukua kati ya miaka 7 na 10 kugundulika.

"Mimi dada yenu hapa ni mhanga wa ugonjwa huu, inaniuma sana, ndoto zangu za kuwa mama zimekwama, naomba serikali iweke mkazo wa kupatikana kwa vifaa vya matibabu ili wasichana na wanawake ambao wengi ni nguvu kazi ya taifa wasipate madhara ambayo mimi nimeyapata na ninaendelea kuumia," alisema mrembo huyo.

Naibu Waziri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Khamisi Kigwangala aliahidi serikali imejipanga kuhakikisha inaboresha sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora na kwa wakati muafaka.

Millen aliongozana na baadhi ya warembo wenzake ambao waliwahi kutwaa taji la Miss Temeke akiwamo, Jokate Mwegelo pamoja na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Judith Wambura 'Lady Jay Dee'.