KLABU ya Kitayosce inayoshiriki Ligi ya Championship imetamba hakuna timu yoyote ya kuizuia kupanda daraja na kusema iko tayari kuonyesha ushindani kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Mwenyekiti wa timu hiyo, Yusuph Kitumbo, amesema msimamo wa Ligi ya Championship unawapa matumaini makubwa ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao na watakachokiangalia ni kukiboresha kikosi ili kijiandae kutoa upinzani.
Kitumbo alizitaka pia timu za Ligi Kuu Bara kujiandaa kukutana na mpinzani mwenye mwenye nguvu na ubora mkubwa.
"Kitayosce tunakwenda kutoa upinzani mkubwa kwenye Ligi Kuu msimu ujao, nina imani hiyo, kwa hiyo wakae mkao wa kula, wakiiona imefika pale wajipange, yaani itakuwa ni shida nyingine imewasili. Atawasili mgeni mwenye nguvu kafika kwenye nyumba ya mwenyeji wake," alitamba Kitumbo.
Mpaka sasa Kitayosce inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi ya Champioship ikiwa na pointi 50, ikisalia mechi nne tu kukamilisha msimu huu.










