Kipanga yageukia kutetea Kombe FA

07Mar 2023
Hawa Abdallah
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kipanga yageukia kutetea Kombe FA

MAAFANDE wa timu ya Kipanga,  wamesema mkakati wao kwa sasa ni kutetea Kombe la Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) maarufu FA Cup, baada ya kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar.

 

Timu ya Kipanga ambao ndio mabingwa watetezi wa Kombe hilo wamesema juhudi na nguvu zao zote wanazihamishia katika michuano hiyo ili kutimiza lengo lao.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa timu hiyo, Swalehe Maalim, alisema licha ya kuendelea na maandalizi ya michezo ya Ligi Kuu Zanzibar ambayo wanahaha kujinasua kushuka daraja, bado wanaendelea na kampeni yao ya kutetea ubingwa wa FA.

Alisema uongozi wa timu hiyo   unatarajia kuwahamasisha wachezaji ili kuhakikisha wanatimiza lengo lao la kutetea Kombe la FA ikiwamo kutoa hamasa hata ya zawaidi iwapo watafanikiwa.

“Kwa upande wetu viongozi, tumejipanga zaidi kuhakikisha tunawahamasisha wachezaji ili kuvumilia hatua hii ya 36 na hatimaye kunyakuwa ubingwa, matumaini yetu hamasa hii itafanikiwa endapo wachezaji watajituma,” alisema.

Michuano ya Kombe la FA hatua ya 36 inatarajiwa kuanza mapema Machi 16, mwaka huu, wakati Maafande wa Kipanga  watakapotupa karata yao dhidi ya Villa FC inayoshiriki Ligi ya Mkoa wa Mjini Magharibi.