Kiduku akiri Msauzi kumzidi, Mandoga atupia ushirikina

01Aug 2023
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kiduku akiri Msauzi kumzidi, Mandoga atupia ushirikina

WAKATI Bondia wa Ngumi za Kulipwa nchini, Twaha Kiduku, akikiri kuzidiwa mambo mengi ya kiufundi na mpinzani wake, Asamahle Wallem kutoka Afrika Kusini na kwamba ndiyo sababu ya kuchezea kichapo juzi, Karim Mandonga yeye ametaja ndumba ndizo zimesababisha kupigwa.

 

Mabondia hao waliopigana walipanda ulingoni jijini Mwanza juzi ambapo Kiduku alikuwa akiwania ubingwa wa WBF dhidi ya Wallem huku Mandonga akichezea kichapo kwa KO dhidi ya Mganda Moses Golola.

Kiduku alipoteza pambano hilo la raundi 12 la uzani wa Super Middle kwa pointi ambapo alikiri hakuwa na siku nzuri kazini dhidi ya mpinzani wake huyo kutoka Afrika Kusini aliyekuwa moto kweli.

Bondia Kiduku alianguka chini katika raundi ya tatu, lakini aliweza kuinuka na kuendelea na pambano hilo baada ya kuhesabiwa ingawa hakuweza kumudu makonde ya mpinzani wake, kutokana na kutawaliwa katika raundi zote kabla ya majaji kumpa ushindi Msauzi huyo, hivyo kushindwa kutetea mkanda wake wa WBF.

Akizungumza baada ya pambano hilo, Kiduku alisema amepoteza pambano hilo kwa kuwa haikuwa siku yake nzuri kazini huku akikiri kuzidiwa mbinu nyingi na mpinzani wake.

"Sikuwa na siku nzuri leo na wala haikuwa bahati, nimepoteza mbele ya mpinzani mzuri ambaye amenizidi mambo mengi, naenda kujipanga naamini nitarudi nikiwa bora zaidi, " alisema Kiduku.

Kwa upande wa Mandonga, alisema ameshindwa dhidi ya Golola, kutokana kuletewa bondia wa ajabu akiwa na waganga wa jadi.

Hilo ni pambano la pili kupoteza kwa Mandonga baada wikiendi iliyopita kupokea kichapo kwa pointi mbele ya Daniel Wanyonyi nchini Kenya.

Alisema haelewi wapinzani ambao amekuwa akiletewa, wengine wamekuwa kama waganga wa kienyeji kutokana na mambo wanayomfanyia kabla ya pambano lenyewe.

"Ni kweli nimepoteza pambano,  binafsi sielewi nimepoteza vipi kwa sababu upande wa mpinzani wangu tangu siku ya kupima uzito nilikuwa simwelewi kabisa, amekuja na mashuka na mikoba kama mganga wa jadi ila niwaambie kwa sasa atakayekuja awe kibwengo au mganga wa jadi, ajue nitapita naye tu bila ya wasiwasi," alisema Mandonga.

Mapambano mengine yaliyopigwa siku hiyo ni Juma Misumali ambaye alifanikiwa kumchapa Paul Kamata wakati Joseph Mchapeni akimshinda kwa TKO raundi ya kwanza Agustine Michael, Ayubu Mwakina amemchapa George Odongo, Mohamed Mkude akimchapa Seba Temba huku Juma Chamamba akishinda kwa TKO ya raundi pili mbele ya James Ebelo.