Kessy: Mayanja ananipatia

07Feb 2016
Lete Raha
Kessy: Mayanja ananipatia

BEKI wa kulia wa klabu ya Simba, Hassan Kessy, amemshukuru kocha Jackson Mayanja kwa kumuamini na kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza na hivyo kuwa chachu ya ushindi katika mechi zao za karibuni.

Kessy alisema atajitahidi kufanya jitihada za kumshawishi kocha kuendelea kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza kwa kuwa ushindani wa namba ndani ya timu ni mkubwa. “Ninajituma nafuata maelekezo ya mwalimu, ndiyo maana nafanya vizuri katika mechi, kikubwa ni nidhamu ya mazoezi,” alisema Kessy. Kessy ambaye alikuwa majeruhi kwa muda mrefu hadi kusababisha kukosa michuano ya Mapinduzi iliyofanyika visiwani Zanzibar, amerudi kwa kasi ya kutishia maisha ya beki kutoka Burundi, Emiry Nimubona, ambaye alikuwa akiikaimu kwa muda nafasi hiyo. Katika mechi alizocheza tangu apone majeraha, Kessy amekuwa mhimili mkubwa hasa akitokea upande wa kulia kwa kupiga krosi ambazo zimeisaidia timu hiyo kupata ushindi ikiwamo kufunga goli lake la kwanza tangu aanze kucheza ligi kuu katika ushindi wa 4-0 dhidi ya African Sport Jumamosi iliyopita.