JKT Tanzania yarejea Ligi Kuu kwa kipigo

24Apr 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
JKT Tanzania yarejea Ligi Kuu kwa kipigo

LICHA ya kuchapwa mabao 3-2 dhidi ya Kitayosce juzi kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, timu ya JKT Tanzania imerejea Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya misimu miwili kupita.

 

Timu hiyo iliyoshuka msimu wa 2020/21, itacheza tena Ligi Kuu msimu ujao wa 2023/24, licha ya kipigo hicho kwenye Ligi ya Championship, na kubakisha mechi mbili.

JKT Tanzania imepanda kutokana na matokeo ya mechi ya Pamba ambayo juzi ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbuni kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Kwa matokeo hayo, pointi 62 ilizonazo  zinaweza kufikiwa na Kitayosce tu kama watashinda mechi zote tatu walizosaliwa nazo, huku Pamba kama itashinda zote itafikisha pointi 61 tu.

Ni timu mbili tu ambazo zinatakiwa kupamba moja kwa moja Ligi Kuu Tanzania Bara, huku mbili zingine zikisubiri hatma yao kwenye mechi za mchujo.

Kitayosce imefanikiwa kutoka na ushindi huo kwa 'hat-trick' ya Moses Nassor dakika ya 31, 44 na 88 iliyoifanya kuwa kwenye nafasi ya pili kwa pointi 53 ikibakisha mechi tatu, huku Pamba baada ya sare ya juzi ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 52.

Baada ya JKT Tanzania kupamba, Kitayosce na Pamba ndizo zinazoonekana kupigana vikumbo kuitafuta nafasi moja ya kupanda moja kwa moja zote zikiwa zimecheza mechi 25 na kubakisha mechi nane.

Kwa maana hiyo hakuna timu yoyote inayotakiwa kupoteza, huku kila moja ikimuombea mwenzake mabaya.

Mechi zingine za Champioship zilizochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Transit Camp ilishinda bao 1-0 dhidi ya Mbeya Kwanza na Fountaine Gate ililazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani, CCM Gairo, Morogoro dhidi ya Mashujaa.