JKT Tanzania imeweka wazi itafanya maboresho katika utawala, benchi la ufundi na kusajili wachezaji wapya ambao watasaidia timu kupambana na ushindani wa mechi za Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu Mkuu wa JKT Tanzania, Abdul Nyumba, alisema kama walivyofanya maandalizi wakati wanashiriki Ligi ya Championships ndio watafanya kuelekea msimu ujao na wanaamini watakuwa imara.
Nyumba alisema wataweka nguvu zaidi katika kikosi chao kwa kufuata ushauri wa benchi la ufundi linaloongozwa na Hamsini Malale.
"JKT Tanzania sio wageni katika Ligi Kuu na sasa tumerejea tena, tutakuja kivingine kabisa, tumeshaamza kujiimarisha kwenye utawala na suala la benchi la ufundi tunasubiri ripoti ya kocha wetu Malale. Kuhusu kocha, bado tunahitaji kuendelea naye kwa sababu amefanikisha timu yetu kupanda Ligi Kuu, hatuwezi kumwacha, lakini tutamsikiliza kana naye atahitaji kuendelea nasi au amepata ofa sehemu nyingine,” alisema Nyumba.
Aliongeza katika usajili wa wachezaji watazingatia nidhamu na viwango vya nyota husika ili kuhakikisha hawashuki tena daraja.










