Shujaa wa Yanga kwenye mechi hiyo alikuwa mshambuliaji Donald Ngoma aliyefunga bao pekee baada ya kazi nzuri ya Juma Abdul.
Matokeo hayo yanawapa nafuu Yanga kwenye mechi ya marudiano wiki mbili zijazo, kwani sasa watahitaji sare ya aina yoyote kusonga mbele.
Iwapo watafuzu kwa hatua ya pili, mabingwa hao wa Bara watakumbana na timu ya APR ya Rwanda au Mbabane Swallows ya Swaziland.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi, Hubert Marie Bruno Andriamiharisoa kutoka Madagascar, Yanga ilipata pigo kipindi cha pili, baada ya mpishi wa bao lake, Juma Abdul kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ilichukuliwa na Pato Ngonyani aliyemalizia vizuri.
Yanga ilitarajiwa kugeuza jana baada ya mchezo huo na itaelekea moja kwa moja Pemba kuweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa.
Kikosi cha Yanga kwenye mchezo huo
Ally Mustafa 'Barthez', Juma Abdul/Pato Ngonyani (dk70), Oscar Joshua, Kelvin Yondan, Vincent Bossou, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Amissi Tambwe/Paul Nonga (dk68) na Deus Kaseke.
Wakati Yanga wakianza vyema michuano hiyo, hapa nyumbani timu ya Mafunzo ya Zanzibar imejiweka katika mazingira magumu ya kusonga mbele baada ya kukubali kipigo cha magoli 3-0 kutoka AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Magoli hayo ya kipindi cha kwanza kwenye Uwanja wa Aman mjini Zanzibar yameiweka kwenye wakati mgumu, kwani sasa wanatakiwa kushinda mabao 4-0 ili kusonga mbele.









