Haaland: Penalti ilinipa wasiwasi sana

07Nov 2022
Na Waandishi Wetu
Dar es salaam
Nipashe
Haaland: Penalti ilinipa wasiwasi sana

ERLING Haaland alielezea penalti yake ya dakika za lala salama dhidi ya Fulham kama "mojawapo ya nyakati nilizokuwa na wasiwasi sana maishani mwangu", alipofunga bao na kuipeleka Manchester City kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England.

 

Mkwaju huo wa penalti uliipa City ushindi wa mabao 2-1 nyumbani Jumamosi baada ya kucheza kwa zaidi ya dakika 64 wakiwa na wachezaji 10 kutokana na kadi nyekundu ya Joao Cancelo.

Haaland, ambaye alianzia benchi baada ya kukosa michezo miwili kutokana na jeraha la mguu, alichukua nafasi ya Julian Alvarez dakika ya 64 na alifunga bao lililokataliwa kwa kuotea kabla ya kuzamisha nyavuni penalti hiyo.

Alvarez alikuwa ameipa City uongozi, lakini Cancelo alipomwangusha Harry Wilson kwenye dakika ya 26 aliipa Fulham penalti na kujipatia kadi nyekundu, hivyo mchezo kubadilika.

Andreas Pereira alisawazisha na City hawakuwa huru katika ushambuliaji wao baada ya hapo.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Haaland alisema: "Ajabu, nilikuwa na wasiwasi. Ulikuwa mojawapo ya wakati wa wasiwasi sana katika maisha yangu.

"Penalti katika dakika ya mwisho, bila shaka ningekuwa na wasiwasi. Lakini ilikuwa hisia ya kushangaza. Sijali jinsi ilivyoingia. Nimekuwa majeruhi kwa wiki moja na ni muhimu sana kushinda."

Mchezaji huyo wa zamani wa Borussia Dortmund, aliyenukuliwa kwenye tovuti rasmi ya City, alisema timu ya Pep Guardiola ilionyesha rangi yao halisi kwa kupambana hadi mwisho ili kunyakua pointi.