Drogba Naye jipu, anaswa kashfa ya ufisadi

17Apr 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Drogba Naye jipu, anaswa kashfa ya ufisadi

GWIJI wa soka wa Chelsea, Didier Drogba, ameingia katika kashfa kubwa baada ya mfuko wake wa hisani kudaiwa kuwatumia watoto wenye uhitaji maalum kwa ajili ya kujinufaisha.

drogba

Mfuko huo unaokwenda kwa jina la Didier Drogba Foundation – ambao unapata sapoti ya David Beckham na Princess Beatrice – umekuwa ukidai kuwasaidia maelfu ya wanafunzi wa Ivory Coast kupata ‘mahitaji muhimu yanayohitajika kwa ajii ya kupata elimu’.

Lakini imebainishwa kuwa ni shule moja tu ambayo vifaa vya masomo – ambavyo ni pamoja na 'notebook' na peni – ndiyo vilitolewa kwa watoto tena wale tu ambao walishiriki video ya tangazo la promosheni ya Mfuko huo.

Mfuko huo wa Drogba pia uliwasafirisha watoto yatima 20 kwa basi hadi kwenye jumba lililoka maili kadhaa kutoka nyumbani kwao, kwa ajili ya kupigwa picha na straika huyo katika siku ya Krismasi kwa ajili ya picha za promosheni ambazo baadaye zilipostiwa kwenye Twitter.

Watoto hao walikula mlo mzuri wa mchana siku hiyo pamoja na mwanasoka huyo na mkewe na watoto wao watatu, wakapewa zawadi na mchezaji huyo na kucheza kwa saa chache kabla ya kurudishwa.

Imebainishwa pia kuwa watoto wengine waliopiga na mwanasoka huyo wa Ivory Coast picha rasmi za kuutangaza mfuko huo si wanufaika kutoka katika Mfuko huo, bali walichukuliwa kutoka Uingereza waigize tu.

Mmoja wa watoto hao ni mjukuu wa mwanasoka maarufu wa England na Arsenal, Ian Wright. Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 7, ambaye alionekana katika tangazo akiwa amevaa fulana ya Mfuko wa Didier Drogba, anaitwa Harvey Wright-Phillips – ni mtoto wa Shaun Wright-Phillips, mchezaji mwenzake Drogba klabuni Chelsea kati ya 2005 na 2008.

Msimamizi wa Mfuko huo, amedai kuwa 'Mfuko umetoa mabegi ya mgongoni 5,000 kwa watoto wa shule’. Aliongeza: ‘Ili kwenda shule, unahitaji peni kuandikia lakini si familia zote zinaweza kumudu gharama hiyo.’

Lakini imebainika kuwa ni watoto wale tu walioshiriki katika video ya promosheni ya Mfuko ndiyo waliopewa mabeki hayo. katika shule ya watoto 800, ni watoto 55 tu waliotokea katika video ya promosheni ndiyo waliopewa begi kila mmoja – na mabegi yenyewe ni ya ubora wa chini sana kwani yamesambaratika baada ya siku chache sana.

Imebainishwa kuwa Mfuko huo unachunguzwa na Umoja wa Mataifa baada ya waandishi wa habari kubaini kwamba umetumia pungufu ya asilimia moja ya pesa zilizochangwa kwa hisani Uingereza katika kuwahudumia watoto hao.

Tangu 2009, ni Paundi 14,115 tu kati ya Paundi milioni 1.7 zilitolewa na wahisani zimetumika katika Mpango wa Mfuko huo.

Takriban Paundi nusu milioni zilitumika katika kuandaa 'pati' za michango ya hisani mjini London, ambapo watu maarufu waliburudishwa na nyota wa pop katika hoteli kubwa. Kiasi kilichobaki kimeachwa katika akaunti za benki kikiwa hakijatumika.

Kuvuja kwa habari hiyo kumewastua wengi hasa kwa kuwa Mfuko huo unaendeshwa na mwanasoka mkubwa duniani, Drogba, ambaye pia ni balozi wa hisani wa Umoja wa Mataifa.

Waangalizi wa hisani wa Uingereza wameanza uchunguzi na ofisa uendeshaji wake, David Holdsworth, wamesema ‘wana shaka kubwa’ na watachunguza kama Mfuko huo ulitoa Foundation ‘provided misleading information to donors and the public’.

Waziri wa Mambo ya Jamii, Rob Wilson, aliongeza kwamba tuhuma hizo 'zinatisha’. Kuna maswali pia kuhusu wapi yamekwenda mamilioni ya paundi ya udhamini kutoka kampuni kubwa za Pepsi, Nike na Samsung, ambazo Drogba amedai zimeenda katika mfumo huo.

Pesa hizi zililipwa moja kwa moka kwenye akaunti ya mfuko huo nchini Ivory Coast.

Mfuko huo ulikataa kubainisha kama mwanasoka huyo alilipa kodi ya mapato kutokana na udhamini huu, alioupata kwa zaidi ya miaka sita wakati akiishi katika jumba lake la kifahari la Paundi milioni 7 (zaidi ya Sh. bilioni 21) lilipo Surrey huku akiichezea Chelsea kwenye klabu ya Ligi Kuu ya England.

Mfuko huo umekataa kuzungumzia tuhuma hizo. Drogba alikanusha kufanya lolote lisilosahihi katika kazi yake ya kusaidia jamii na akasisitiza kwamba 'anajitoa' kikamilifu kusaidia yatima nchini Ivory Coast.