Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge kwenye mbio za Coast City Marathon zilizofanyika Kibaha amesema katika mkoa huo vifo vya uzazi vimepungua kutoka vitano vya mwaka 2021 hadi vitatu kwa mwaka 2023.
Akihutubia wananchi walioshiriki katika mbio hizo zenye lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tumbi Kunenge amesema hadi sasa malengo yanaenda kufikiwa na juhudi zitaendelea ili vifo hivyo visitokee kabisa.
Akizungumzia kuhusiana na Hospitali ya Rufaa ya Tumbi Kunenge amesema jengo hilo ni muhimu kutokana na ongezeko la wagonjwa wanaopata huduma.
Kunenge amesema kwasasa Hospitali ya Rufaa Tumbi inatoa huduma bora na matibabu zikiwemo za kuchuja figo, vipimo vya CT- Scan, ujuzi kwa wataalam wa afya na wajawazito.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa Hospitali hiyo inapokea wagonjwa 500 kwa siku na 2,081 kwa mwezi ambao wanakutoka maeneo mbalimbali lakini pia wagonjwa 24000 kwa mwaka na 200 kwa mwezi katika wodi ya wazazi na kuna vitanda vitatu vya kulaza wagonjwa.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Dk. Amani Malima amesema mbio hizo ni kampeni ya kukusanya fedha kutoka kwa wadau mbalimbali zikiwemo taasisi binafsi na serikali.
Amesema jengo la wodi ya wazazi limeelemewa na wagonjwa na hivyo kuomba msaada wa jengo lingine ambalo lisaidia kuhudumia wangonjwa wengi kwa wakati mmoja na kwamba ili kufanikisha ujenzi wa jengo jipya kiasi cha sh milioni 240 kinahitaji.
Mratibu wa mbio hizo Frank Muhamba amesema zaidi ya sh miln. 10 zimekusanywa na uhamasishaji unaendelea kwa wadau mbalimbali ili kufikia lengo.
Takwimu za vifo vya mama na mtoto katika Mkoa wa Pwani inadaiwa kupungua kutoka vitano kwa mwaka 2021 hadi vitatu kwa mwaka huu ambapo lengo ni kutokuwa na kifo kwa kipindi kijacho.










