Cheka, Ajetovic ngumi nzito leo

27Feb 2016
Dar
Nipashe
Cheka, Ajetovic ngumi nzito leo

BONDIA Francis Cheka ametakiwa kupunguza uzito wa kilo mbili ili apigane na Geard Ajetovic katika pambano la kuwania ubingwa wa mabara linalotambuliwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa (WBF) kwenye Viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam leo.

Ajetovic, akizumgumza na waandishi wa habari.

Baada ya mabondia hao kupima afya jana, Cheka aligundulika kuwa na uzito kilo mbili zaidi na kutakiwa kupunguza kufikia kg 76 za mpinzani wake huyo kutoka Serbia.

Rais wa WBF, Howard Goldberg, alisema baada ya kumalizika kwa taratibu za vipimo kuwa Cheka ana wakati mgumu wa kupunguza uzito huo ili amfikie mpinzani wake na kuruhusiwa kupanda ulingoni.

"Cheka atakuwa kwenye mazingira magumu ya kushinda, wakati mpinzani wake sasa anapumzika kusubiri pambano, yeye anatumia nguvu nyingi kukata kilo, jambo ambalo kiafya linaweza kumuathiri," alisema bosi huyo wa ngumi wa WBF.

Alisema mazoezi ambayo Cheka alilazimika kufanya kuanzia jana ili kufikia uzito unaotakiwa, yatamchosha na huenda yakaufanya mwili wake ukashindwa kumudu raundi 12 za pambano hilo la kimataifa.

Mapambano ya utangulizi leo yatakuwa ni kati ya Cosmas Cheka dhidi ya Mustapha Dotto ambalo litakuwa la kuwania mkanda wa WBF uzito wa Super Middle wakati Mohamed Matumla atazichapa na Bakari Mohamed kwenye uzito mwepesi.

Bakari Mwakansope atazidunda na Shaaban Kaoneka (uzito wa kati- raundi nane) huku kwa upande wa wanawake Lulu Kayage atachuana na Mwanne Haji huku mgeni rasmi katika pambano hilo akiwa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.