Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema tayari chama chake kimeshaandaa utaratibu wa kuanza kukarabati viwanja hivyo ambavyo vingi vinatumika katika michezo ya Ligi Kuu ya soka Bara.
Nauye ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alisema tayari vikao vya ndani vya CCM vimeshapita na utekelezaji wa ujenzi utaanza wakati wowote kuanzia sasa.
"Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa na mimi nipo kule (CCM), hili la ukarabati na matengenezo tumeshaliona na utekelezaji wake utaanza hivi karibuni, tunakiri hali iliyoko sasa si nzuri," alisema Waziri Nnauye wakati akisoma risala yake kwa Waziri Mkuu Majaliwa juzi alipokutana na viongozi wa vyama mbalimbali vya michezo hapa nchini.
Aliongeza kuwa miundombinu inapokuwa bora, wanamichezo wanapata nafasi ya kufanya maandalizi yao kwa ajili ya kushindana katika mashindano mbalimbali na kuacha kuwa wasindikizaji kwenye michuano ya kimataifa.
CCM inamiliki viwanja mbalimbali nchini na baadhi ni CCM Kirumba (Mwanza), CCM Mkwakwani (Tabora), Jamhuri (Dodoma), Jamhuri (Morogoro) na Ali Hassan Mwinyi (Tabora).









