Kwenye Uwanja wa Marrakech, Simba iliruhusu bao dakika za majeruhi lililowekwa wavuni na Zakaria Draoui na kuifanya kuburuza mkia kwenye Kundi B ikiwa na pointi mbili, linaloongozwa na Asec Mimosas yenye pointi saba, ambayo ilishinda ugenini nchini Botwasana dhidi ya Jwaneng Galaxy kwa mabao 2-0.
Benchikha amesema yote yaliyotokea anakwenda kuwapa usahihi wa maandalizi ya mechi ijayo, huku akisema bado timu yake ina nafasi kutokana na kundi jinsi lilivyo.
"Yote yaliyotokea hapa yatakwenda kutupa usahihi wa maandalizi mazuri ya mchezo ujao. Eneo tulilokuwa bora tutakwenda kuongeza ili kuimarika zaidi na kwenye mapungufu tutakwenda kuparekebisha," alisema kocha huyo, ambaye pamoja na kupoteza, wanachama na mashabiki wa Simba wameonekana kuridhishwa na kiwango cha timu yao, hivyo kuwa na imani naye hasa timu itakapofanya usajili wa kuongeza baadhi ya wachezaji kipindi cha dirisha dogo.
Kocha huyo alisema bado ana kazi ya kufanya ili kuwajenga wachezaji ambao aliwakuta wana matatizo mengi, ikiwamo kutokuwa na utimamu wa mwili, kukata tamaa na kutojiamini.
Meneja Habari wa Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema timu yao imepoteza mechi ikiwa kwenye kilele cha ubora wao.
Alisema walikuwa vizuri kwenye kila kitu, lakini tatizo hawakuwa vizuri katika kutumia nafasi walizozipata.
"Tulikuwa vizuri kwenye kumiliki mpira, kupiga pasi, tulikaba vizuri, na tulikuwa vizuri kwenye kujenga mashambulizi, ila hatukuwa vizuri kutumia nafasi tulizozipata, mazuri yote tunaondoka nayo kwa ajili ya mechi ijayo na udhaifu tutaufanyia kazi ili Desemba 19 tuwe bora kwenye kutumia nafasi.
"Kwenye kilele cha ubora wetu, tunapoteza mchezo, kazi nzuri wachezaji wetu, mmepambana na kuvuja jasho kwa ajili ya timu yetu, lakini dakika za nyongeza zimekuwa katili kwetu, kwa sasa hatima yetu ipo mikononi mwetu Desemba 19 tunamkaribisha Wydad kwenye tanuru la moto Benjamin Mkapa," alisema Ahmed.
Tarehe hiyo ambayo itakuwa Jumanne ya wiki ijayo, Simba itashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa, saa 10 jioni kucheza mechi ya raundi ya nne ambayo itaonesha dira ya timu hiyo ya Tanzania kama inaweza kufanikiwa kwenda hatua ya robo fainali msimu huu au la.
Kwa misimu minne, tangu 2019, timu hiyo haijawahi kuishia hatua ya makundi, badala yake imekuwa ikitinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.










