Benchikha atoa sababu Simba kukosa ushindi Botswana

05Dec 2023
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Benchikha atoa sababu Simba kukosa ushindi Botswana

KOCHA Mkuu wa Simba, Mualgeria Abdelhak Benchikha, amesema wachezaji wake kutokuwa na kasi, hasa mita 30 kabla ya kulifikia lango la wapinzani wao, ndicho kilichowanyima ushindi kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi iliyochezwa jumamosi dhidi ya Jwaneng Galaxy, Uwanja wa-

KOCHA Mkuu wa Simba, Mualgeria Abdelhak Benchikha.

-Obed Itani Chilume, jijini Francistown, Botswana.

Benchikha alisema wachezaji wake hasa washambuliaji na viungo wake hawakuwa na kasi wanapolikaribia lango la mpinzani wao, hivyo kuwapa urahisi mabeki wa timu pinzani kuokoa na kusoma mienendo yao. 

"Ilikuwa mechi nzuri kiukweli, tumekosa pointi tatu licha ya kucheza vizuri. Mita 30 kabla ya lango la Jwaneng Galaxy hatukucheza kwa kasi ya kushambulia na tumepoteza mabao mengi kutokana na kutokuwa na ufanisi, sijui kama niwe na furaha au nisiwe nayo kwa sababu pointi moja sifikiri kama ni nzuri kwetu, hasa baada ya mechi iliyopita dhidi ya Asec Mimosas," alisema kocha huyo aliyekuwa akiiongoza Simba kwa mara ya kwanza.

Kocha huyo aliwasifu wapinzani wao kutokana na mpango mkakati walioingia nao uwanjani, wakiwaachia mpira, wakikaa nyuma na kushambulia kwa kushtukiza.

"Tumepoteza pointi mbili nyumbani na leo tumepoteza pointi mbili ugenini, ila mwisho kabisa nasema sipendezwi na hali hii.

Jwaneng Galaxy ni timu nzuri inayoonyesha nini inakihitaji, walituacha sisi tumiliki mpira na wakawa wanatushambulia kwa kushtukiza, mpango wao ulikuwa mzuri, wana wachezaji wazuri pia, ila naweza kusema mpaka sasa kundi bado liko wazi, tutakwenda kuwekana sawa ili tuangalie mechi zijazo tunachezaje," alisema kocha huyo.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally alisema pamoja na kukosa matokeo ya ushindi, lakini kwa mara ya kwanza timu yao imecheza kwa kiwango kikubwa chini ya kocha Benchikha.

"Si matokeo mabaya sana na wala si mazuri ya kujivunia, tulikuwa na nafasi kubwa ya kupata ushindi, nadhani katika mechi zote tulizocheza msimu huu za mshindano yote, leo (juzi) ndiyo tumecheza kwa kiwango cha juu sana.

"Timu inatia matumanini hasa baada ya ujio wa mwalimu, kinachotufanya tusiwe na tabasamu ni kukosa tu ushindi lakini si kiwango," alisema Ahmed.

Kwa matokeo hayo, Simba inashika nafasi ya tatu kwenye Kundi B, ikiwa na pointi mbili mpaka sasa na bao moja, baada ya juzi usiku Asec Mimosas kuifunga Wydad bao 1-0, hivyo Waivory Coast hao wanaongoza kwa pointi nne na mabao mawili, Jwaneng Galaxy ikishika nafasi ya pili kwa pointi nne na bao moja, huku Wydad ikishika mkia ikiwa haina pointi wala bao.