Taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga jana, imesema Doumbia aliondoka nchini jana kuelekea kwao Mali kwa ajili ya kushiriki taratibu za mazishi, na hivyo ataukosa mchezo huo mkubwa.
Mchezaji huyo ambaye alisajiliwa kipindi cha dirisha dogo, hakupata nafasi ya kucheza katika mechi kadhaa, kabla ya kupata nafasi hiyo kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar.
"Klabu ya Yanga imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha baba mzazi wa mchezaji wetu, Mamamou Doumbia, kilichotokea jana (juzi) nchini Mali.
Doumbia anatarajia kusafiri asubuhi leo (jana), kuelekea Mali kwa ajili ya taratibu za mazishi. Kwa niaba ya wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga, uongozi wa Yanga unatoa pole kwa mchezaji wetu, Doumbia na familia yake yote kwa msiba huo na Mwenyezi Mungu awatie nguvu katika kipindi hiki kigumu." Ilimaliza sehemu ya taarifa hiyo ya klabu hiyo.
Hata hivyo, haitokuwa tatizo katika kikosi hicho kutokana na nyota huyo bado hajaingia kwenye mfumo wa kuaminiwa moja kwa moja, hivyo ukuta wa kati Yanga utaendelea kuongozwa na Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Abdallah 'Bacca' na Yannick Bangala.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga watashuka dimbani kuwavaa Simba wakiwa ndio vinara wa ligi hiyo na msimu hii ikiwa imetinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Pia itashuka katika mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 5-0 walioupata dhidi ya Kagera Sugar.










