Bangala awashusha presha mashabiki Yanga

30Jun 2023
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Bangala awashusha presha mashabiki Yanga
  • Asema bado ana mkataba wa mwaka mmoja na mabingwa hao, aahidi kujituma na kushirikiana...

BAADA ya tetesi kuwa huenda kiungo wa Yanga, Yanick Bangala, atatimka kwenye kikosi cha timu hiyo, nyota huyo amesema bado ataendelea kuwapo Jangwani kwa kuwa ana mkataba mmoja zaidi na mabingwa hao wa soka nchini.

Yanick Bangala.

Bangala pamoja na nyota wengine wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndani ya Yanga, alikuwa akihusishwa kutaka kuondoka ndani ya timu hiyo huku akihusishwa kutaka kujiunga na matajiri wa Chamazi, Azam FC.

Akizungumza na Nipashe, Bangala alisema, anawashukuru mashabiki wa Yanga kwa sababu siku chache zilizopita yaliibuka mengi kuhusu hali yake na klabu hiyo anayoitumikia lakini bado alikuwa imara na kuweka imani yao kwa timu.

“Yamesemwa mengi sana, lakini nawahakikishia wanayanga mimi bado nina mkataba na klabu yangu mpaka mwakani, nitaendelea kuheshimu mkataba wangu,” alisema Bangala.

Alisema anafahamu kipindi hiki cha usajili na yatazungumzwa mengi sana juu ya mustakabali wa wachezaji lakini yeye bado ni mchezaji halali wa Yanga na yupo tayari kuitumikia msimu ujao.

“Nimewekeza nguvu na akili zangu kwa asilimia 100 kuhakikisha tunafikia malengo yetu, tulifanya vizuri msimu uliomalizika na sasa tunajiandaa kwa ajili ya msimu ujao binafsi nitakuwa bega kwa bega na benchi jipya la ufundi,” alisema Bangala.

Aliongeza kuwa ana uhakika atapambana na kuwapa ushirikiano mkubwa makocha wapya ili kufikia malengo yao ikiwamo kutwaa mataji yote ya ndani na kuleta kombe la Afrika.

“Msimu huu tunataka kufanya vizuri zaidi na kwa kuwa tulifika fainali ya Kombe la Shirikisho basi malengo yetu itakuwa kutwaa ubingwa wa Afrika na kuleta kombe Tanzania, hii inawezekana tukiwa na malengo ya pamoja na kushirikiana vyema,” alisema Bangala.

Baada ya ligi kumalizika, Bangala pamoja na Wakongo wenzake, Shaaban Djuma na Joyce Lomalisa walihusishwa kutaka kuondoka ndani ya klabu hiyo na kushinikiza uongozi uwaboreshee maslahi ili waendelee kuwamo kwenye kikosi cha Yanga msimu ujao.