Azam yainolea makali Simba

26Apr 2023
Saada Akida
DAR ES SALAAM
Nipashe
Azam yainolea makali Simba

KOCHA Msaidizi wa Azam FC, Kalimangonga Ongala ameanza mikakati ya kuimarisha safu ya ushambuliaji kuelekea nusu fainali ya kombe la Shirikisho Tanzania, FA, dhidi ya Simba.

 

Safu ya ushambuliaji ya Azam inaongozwa na Prince Dube na  Idrissa Mbombo na sasa wamepewa jukumu la kuhakikisha wanaiondoa Simba katika michuano hiyo.

Pia safu ya ulinzi nayo inanolewa ili kuwa makini zaidi kwa sababu wameona ubora wa Simba katika safu ya ushambuliaji ambayo ni hatari na wako makini wanapopata nafasi.

Azam watakuwa wenyeji wa Simba katika nusu fainali hiyo Mei 5 mwaka huu katika dimba la Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Akizungumza na Nipashe jana, Ongala alisema amekuwa akiwafuatilia Simba katika mechi wanazocheza na kuona ubora wao hasa safu ya ushambuliaji na hivyo wanaendelea kujipanga.

Alisema mchezo huo utakuwa mgumu kwa sababu uwanja wanaokwenda kuutumia wote watakuwa ugenini hali hiyo haitakuwa na kisingizio endapo mmoja wapo atapoteza .

“Hatuhitaji sababu kwa kuwa Nangwanda Sijaona wote ni wageni, uwanja, kikubwa tunaendelea kujiimarisha na kufanyia kazi kikosi chetu ikiwemo safu ya ushambuliaji na ulinzi kwa kuangalia ubora wa wapinzani wetu,” alisema Kalimangonga.

Aliongeza kuwa kitendo cha kumuanzisha Mbombo katika mechi mbili mfululizo huku Dube akitokea benchi ni kwa ajili ya mipango yao na sio sababu ya kumpumzisha (Prince) kwa ajili ya Simba.

“Sio kweli Dube amepumzishwa kwa ajili ya mechi ya Simba au tunamuandaa Mbombo bali tunafanya mabadiliko ya safu ya ushambuliaji kulingana na wapinzani tunaokwenda kukutana nao, kwa mechi ya Simba tunaenda kujiandaa vizuri,” alisema.

Aliongeza: “Tunahitaji kupambana kutafuta matokeo katika mchezo wetu huo wa nusu fainali, na naamini mechi itakuwa ngumu kwa sababu Simba tuliwafunga katika ligi na hawatakubali kupoteza kwa mara nyingi hasa ukizingatia huu mchezo akifungwa mmoja anaondolewa kwenye mashindano,” alisema Kalimangonga.

Alisema wanahitaji kupambana katika matokeo hayo ili kubadilisha mwenendo mzuri kwa Azam kwa msimu huu baada ya kushindwa kufikia malengo yao katika Ligi Kuu Tanzania Bara.