Amesema anasahihisha makosa yao kwenye safu ya ulinzi na ushambuliaji ili kuwa makini katika mchezo ujao watakaocheza na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga.
Akizungumza na Nipashe, Dabo amesema baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Coastal Union, wamerejea katika uwanja wa mazoezi kwa ajili ya kusahihisha baadhi ya makosa yao.
Amesema sehemu zote zilikuwa na makosa, safu ya ulinzi na ushambuliaji, ameelekeza umakini wake katika maeneo hayo kwa sababu mechi inayofuata wanazitaka pointi tatu kwa kutowapa wapinzani nafasi ya kufanya mashambulizi.
“Washambuliaji nao wanatakiwa kuwa makini hasa nafasi tunazotengeneza, tunapoteza nafasi nyingi, katika hilo tunafanyia kazi kujiandaa na mchezo wetu unaofuata dhidi ya Yanga,” amesema kocha huyo.
Ameongeza kuwa, wanachoangalia zaidi ni kutafuta pointi katika kila mchezo uliopo mbele yao ili kufikia malengo yao pamoja na mashabiki kuona timu yao inacheza mpira mzuri na kupata matokeo mazuri.
Jumapili wiki hii, Azam FC watakuwa nyumbani katika mchezo wa mzunguko wa pili wa ligi hiyo ikiwakaribisha Yanga, kwenye dimba la Azam Complex lililopo Chamazi jijini Dar es Salaam.