Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana kwenye hoteli ya Collessium, barabara ya Nyerere, Dar es Salaam, Aveva alisema wachezaji hao walifanya vitendo ambavyo vimewaondolea uaminifu katika klabu.
Aveva alisema Kessy alitolewa kwa kadi nyekundu katika mechi ya Ligi Kuu na baada ya adhabu hiyo, klabu ikaamua kumuongezea adhabu, lakini kabla hajamaliza adhabu zake akaibuka anasaini kwa mahasimu Yanga.
Kuhusu Ajib, Aveva alisema mshambuliaji huyo alitolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi Kuu pia na asubuhi yake akapanda ndege kwenda Afrika Kusini.
Alisema mambo kama hayo pamoja na uendeshwaji mbovu wa Ligi Kuu unaofanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) vimechangia Simba kufanya vibaya msimu huu.
Aveva alisema kutakuwa na Mkutano Mkuu wa klabu Julai 10, mwaka huu kujadili matatizo ya klabu na kutafuta suluhisho lake.
Kauli ya Aveva inakuja Ajib akiwa amefuzu majaribio katika klabu ya Lamontville Golden Arrows FC ya Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini.
Hata hivyo, klabu hiyo haiko tayari kumnunua mchezaji huyo bali inataka kumchukua kama mchezaji huru na kumsainisha mkataba.
Kwa sababu hiyo, klabu hiyo imemuambia Ajib arejee Dar es Salaam kuangalia kama mkataba wake umekwisha apeleke uthibitisho Afrika Kusini ili apewe mkataba Arros.
Wakala wa mchezaji huyo, Juma Ndabila, ameiambia Lete Raha kwamba wanarejea leo Dar es Salaam pamoja na Hajib.
“Amefuzu majaribio, lakini kuna suala la mkataba hapa, yeye alisema kamaliza mkataba, na Simba wanasema bado ana mkataba, kwa hivyo anarudi kutatua hilo suala,” alisema Ndabila.
Kwa upande wake, wakala aliyemuunganishia majaribio Ajib Afrika Kusini, Rodgers Mathaba alisema kwamba mchezaji huyo amepewa fursa ya kurudi Arrow wakati wowote akiwa mchezaji huru.
“Amefuzu majaribio, sasa ni juu yake anatakiwa hapa kama mchezaji huru, anarudi Dar es Salaam kushughulikia mkataba wake, nafasi yake ipo wazi hapa wakati wowote,” alisema Mathaba.










