Acacia, Sunderland watenga mil 462 kuinua michezo

01Apr 2016
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Acacia, Sunderland watenga mil 462 kuinua michezo

BAADA ya kufanikisha ujenzi wa kituo cha michezo cha Kidongo Chekundu, Dar es Salaam, Klabu ya Sunderland ya Uingereza kwa kushirikiana na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Acacia wametenga Sh. milioni 462 kuendeleza michezo nchini.

Moja ya kiwanja kilichopo katika kituo hicho.

Mkuu wa Kitengo cha Kuendeleza Michezo wa Sunderland, Graham Robinson, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa kiasi hicho cha fedha kitatumika kusaidia kukuza michezo kwa kutoa mafunzo kwa wachezaji wa shule za msingi na kozi kwa walimu vijana.

Deo Mwanyika, Makamu wa Rais wa Acacia - Uhusiano, alisema ubia wao huo na Sunderland ni sehemu ya mchango wao kwa jamii na maendeleo ya taifa.

"Sisi (Acacia) tunaidhamini klabu ya Stand United inayoshiriki ligi kubwa ya Tanzania. Tumeona kuna haja ya kutoa fursa kwa vijana maana msingi wa maendeleo ya mchezo wowote tunaamini unapaswa kujengwa kuanzia kwa watoto wadogo," alisema.

Mkurugenzi wa Biashara wa Sunderland, Gray Hutchinson, alisema klabu hiyo inajivunia kukamilisha ujenzi wa kituo cha Kidongo Chekundu kwa kushirikiana na kampuni ya kufua umeme ya Symbion Power.

"Katika ubia huu wa miaka miwili na Acacia, tunatarajia kutoa mafunzo ya michezo mbalimbali kwa makocha vijana na wanafunzi wa shule za msingi wa maeneo ambako Acacia wanachimba madini nchini Tanzania. Tutatumia pauni 150,000 (milioni 462.3) katika mpango huu," alisema Hutchinson.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, aliupongeza uongozi wa Acacia na Sunderland kwa kuamua kusaidia sekta ya michezo nchini huku akiahidi kuupa ushirikiano katika masuala yanayohusu mpira wa miguu.

Imeandikwa na Sanula Athanas na Renatha Msungu