Wiki hii, Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema kwamba ameuandikia barua uongozi wa Yanga SC kutaka ufafanuzi wa kile kinachoripotiwa kuhusu Bodi ya Wadhamini kuingia mkataba wa kuikodisha kwa Kampuni ijulikanayo kwa jina la Yanga Yetu Limited.
Kimsingi inasema TFF haipingi mabadiliko ya aina yoyote, badala yake inataka kujua kama taratibu hasa zinazohusiana kisheria kama zimefuatwa – hivyo sasa imeitisha mkataba huo kutoka kwa Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit ili kuona kile kinachoelezwa kuhusu mfumo wa uendeshwaji na umiliki wa klabu hiyo yenye zaidi ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwake.
TFF imesema kwamba kwa sasa haitambui mabadiliko yoyote hadi hapo itakapopewa taarifa rasmi ya maandishi kutoka kwa uongozi wa klabu hiyo.
Na hatua ya TFF kuomba ufafanuzi imefuatia kupokea barua mfululizo kutoka kwa wadau mbalimbali wa Yanga wakihoji taratibu au hatua zinazoendelea katika mfumo wa umiliki na uendeshwaji wa timu hiyo.
Na hayo yalikuja baada ya Yanga kutoa muhtasari wa Mkataba wa kuikodisha timu kwa kampuni ya Yanga Yetu Limited.
Mbali ya misukumo hiyo, TFF imesema pia haikuridhishwa na majibu ya Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Bakara Deusdedit ambaye alipoandikiwa barua kwa mara ya kwanza Agosti 30, 2016 alijibu kwamba Bodi ya Udhamini ndiyo ina majibu.
Mwesigwa alisema wanataka kuona kilichopo kwenye mkataba kabla ya kushauri uongozi wa Yanga ili kuangalia kama vinakwenda sambamba na matakwa ya TFF, CAF na FIFA ili kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakiendelea kwani wengine wamefika hatua ya kuomba idhini ya TFF hata kwenda kuwaona viongozi wa Serikali.
Mwesigwa alisema wanataka kujua pia nani anamiliki na nani anaendesha timu na umiliki wake ukoje kwa maana hizi timu za Simba na Yanga zinagusa nyoyo za watu wengi na taratibu za uhamishaji umiliki wake ukawa wa wazi-hadharani.
Alisema kubadilisha uendeshwaji inatakiwa kufuata taratibu ikiwa ni pamoja kuenenda sawa na katiba ya klabu, kamati ya utendaji ifahamu, mkutano mkuu uridhie ili kujua nini kinauzwa na nini kinakodishwa ikiwa ni kwenye level (hatua) ya klabu.
Alisema kama itakuwa nje ya utaratibu wa TFF wa uendeshaji wa klabu wa Kamati ya Sheria na Kamati ya Utendaji watafanya kazi na kama watakuwa wamefuata taratibu inaweza isifike huko kwenye CAF na FIFA.
Mwesigwa alisema TFF itaendelea kuwasiliana na Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit au viongozi wakuu ili kupata maelekezo.
Tayari Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia kwa Katibu wake, Mohammed Kiganja limesema halitambui klabu ya Yanga SC kukodishwa kwa kampuni ya Yanga Yetu, kwa kuwa taratibu hazikufuatwa na Baraza la Wadhamini la klabu hiyo halitambuliki.
Kiganja alisema wiki iliyopita kati ya Wajumbe wa Baraza la Wadhamini la Yanga lililoundwa Julai 5, mwaka 1973 ni wawili tu wanaotambulika na walio hai hadi sasa, ambao ni Dk. Jabir Idrisa Katundu na Juma Mwambelo, ambaye kwa sasa hajihusishi na masuala ya klabu hiyo, wakati wengine wamekwishafariki dunia.
Alisema ili Yanga ikodishwe, inatakiwa kwanza kifanyike kikao cha Kamati ya Utendaji itakayochambua hoja na kukubaliana au kutokukubaliana kabla ya kwenda kwenye Mkutano Mkuu wa wanachama, uwe wa dharura au kawaida na maamuzi yatakayofikiwa katika Mkutano yatapelekwa Baraza la Wadhamini, ambalo ndilo litawasilisha suala hilo kwa Msajili.
Alisema sheria ya BMT ya mwaka 1967 kifungu namba 11 (1) inasema chama chochote kinachofanya mabadiliko ya jina, anuani, madhumuni au kifungu chochote cha Katiba yake kitatakiwa kiidhinishwe ya Msajili wakati Kifungu namba 11 (3) Msajili anaweza kuyakataa maombi ya kubadili kifungu chochote cha Katiba kama ataona kuwa mabadiliko yanaweza kuhatarisha usalama na kuvuruga amani, au kama kuna malengo ya kuwanufaisha wachache au kama hayazingatii sera za michezo na sheria za BMT.
BMT wametilia shaka mchakato wa Yanga kukodishwa kwamba haukufuata taratibu, lakini TFF inataka barua na vielelezo vya mchakato hadi kufika hapa.
Suala la mabadiliko ya mfumo wa uendeshwaji kwa klabu kongwe kama Yanga si dogo, linahitaji ushirikishwaji wa vyombo hivyo vikubwa vya michezo nchini kikamilifu, TFF na BMT.
Ndiyo maana leo Nipashe tunawaambia viongozi wa Yanga wawape ushirikiano TFF na BMT katika suala la ukodishwaji wa timu.










