W/biashara wachangamkie fursa za biashara nchi jirani

30Nov 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
W/biashara wachangamkie fursa za biashara nchi jirani

JUZI Rais Samia Suluhu Hassan alieleza kuwa vikwazo vilivyokuwapo baina ya  Tanzania, Kenya na Uganda vilivyodhorotesha biashara vimeondoka, hivyo sasa ni wakati wa wafanyabiashara kuchangamkia fursa, ili kuimarisha uchumi wao na nchi zao.

Alieleza kuwa kutokana na vikwazo hivyo, biashara baina ya nchi hizo ilikuwa ngumu kiasi cha kufikia bidhaa kutoruhusiwa kuvuka mpaka, huku vifaranga kutoka Kenya vikichomwa moto na sukari kutoka Uganda kutoruhusiwa kuingia nchini.

Hali hiyo ilisababisha kila upande kuweka zuio dhidi ya mwingine kwa kuwa viongozi wa maeneo ya mpakani kuwa na uadui ambao uliathiri nchi zote kwa kuwa biashara nyingi zilizuiwa kuingai nchi husika.

Rais alisema kwa sasa vikwazo vyote vimemalizika baada ya kuwapo mazungumzo ya pande zote na sasa ni wakati wa kila upande kuchangamkia biashara ili kudumisha ushirikiano na kunufaisha nchi kiuchumi na kutoa ajira za moja kwa moja na za muda mfupi.

Tunatambua nchi hizi ni Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambao wamekubaliana kupunguza vikwazo vya kibiashara kiasi cha kuondoa baadhi ya masharti kwenye mipaka ili kurahisisha biashara baina ya nchi wanachama wa jumuiya.

Kupitia umoja huo nchi hizo zilifikia mahali pa kujadili uwezekano wa kuwa na pasi moja ya kusafiria, umiliki wa ardhi, kuondoa vikwazo vya biashara katika kuelekea katika shirikisho na kuongozwa kuwa na kiongozi mmoja.

Panapojitokeza tofauti ambazo zinasababisha kutokuelewana ni muhimu zikashughulikiwa mapema kabla ya kusababisha madhara makubwa kwa wananchi kama ilivyojitokeza hadi nchi kuwekeana vikwazo kwamba bidhaa za upande huu hazitapita na za huku hazitapita.

Hili linakumbusha jinsi Kenya ilivyotangaza kuwa mahindi kutoka Tanzania yana sumu kuvu, hivyo hayaruhusiwi kuingia nchini humo, kiasi cha magari mengi kukwama kwenye mipaka ya Namanga, Sirasi, Tarakea, Holili na Horohoro.

Baada ya mazungumzo ya viongozi wa pande zote, hali ilirejea na haikuelezwa tena kwamba mazao hayo yameacha kuwa na sumu iliyokuwa inatwaja, jambo linalodhihirisha kuwa kulikuwa na mvutano unaoendelea ambao ulitingisha uhusiano wa nchi husika.

Tunatarajia kuona kuimarika kwa biashara baina ya nchi husika kwa kuwa vikwazo vimeondolewa, na wakuu wa nchi hizo wameridhia kushirikiana na kufanya biashara zenye manufaa.

Ni wakati muafaka sasa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuona fursa nyingi zilizoko Uganda kwa kupeleka bidhaa, kufungua kampuni na ofisi mbalimbali nchini humo ambazo zitaendelea kuzitangaza bidhaa zinazozalishwa nchini.

Kuimarika kwa biashara baina ya nchi na nchi kunasaidia kuboresha uhusiano, kuingizia nchi fedha za kigeni, kuongeza wawekezaji na kukuza uchumi kwa kuwa watu watapata ajira za muda mfupi na za kudumu, mzunguko wa fedha utaongezeka na maendeleo ya miundombinu na watu yataongezeka.

Kutokana na mgawanyiko wa kijiografia nchi zinategemea na kwa mambo mengi kwa kuwa raslimali zipo kwenye nchi tofati na hakuna iliyojitosheleza kwa kila kitu, na ndiyo maana mpaka unapofungwa wananchi wa nchi fulani wanataabika kwa kukosa mahitaji muhimu ikiwamo chakula.

Tunaipongeza serikali kwa kushughulikia kasoro zilizojitokeza na tunaamini imejengwa misingi imara itakayozuia kujirudia tena, sasa ni wakati wa biashara kustawi baina ya nchi na nchi.

Wafanyabiashara wa Tanzania wasibaki nyuma katika kuchangamkia fursa ili isiwe ni wafanyabiashara kutoka nje wanafanya biashara kubwa bali tuone Watanzania wakiwekeza na kuwa na biashara kubwa zenye kuajiri mamia katika nchi hizo.

Pia wachangamkie biashara ya nchi na nchi inayoletwa na fursa mbalimbali, ikiwamo manufaa ya mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga.

Haitarajiwi kuona vyakula vinatolewa nje bali kampuni zinunue bidhaa zinazozalishwa na Watanzania wenyewe na ajira zitakuwa kipaumbele kwa wazawa ambako mradi unatekelezwa.