Fedha hizo ni Dola za Marekani bilioni 576 ( Sh. trilioni 1.3) ambazo zitaelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya afya, maji na elimu ambayo inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja, na lengo ni kuboresha maisha yao na kukuza uchumi wa nchi.
Rais alisema kuna tabia baada ya fedha kupatikana watu wanaunda kamati ambazo huwa ni kichaka cha kujipatia fedha, na kuonya uundwaji wa kamati hizo kuwa kwa umakini kwa kuwa na wataalamu watekelezaji na siyo watu wa kujipatia fedha.
Aidha, aliagiza kila mkoa kuwa na timu ya ufuatiliaji wa miradi husika ambayo moja kwa moja itaulizwa juu ya utekelezaji wake, ili kuepuka kuwa na timu nyingi kwa maana ya ngazi ya mkoa na wilaya.
Rais alitoa kauli hiyo kwa msisitizo kuonyesha ni kwa kiasi gani anakerwa na matumizi mabaya ya fedha za umma, huku fedha nyingi ikielekezwa kwenye kugharamia posho na matumizi mengine na kiduchu ikiwafikia wananchi kupitia miradi ya maendeleo.
Hakuna ubishi kuwa mshirika wa maendeleo yeyote anapotoa fedha anataka kuona zinawafikia wananchi moja kwa moja na kuleta matokeo kwa maana ya kubadilisha maisha yao, lakini imekuwa desturi kuwa sehemu kubwa ya fedha inatumika kugharamia posho, vyakula na gharama nyingine ambazo kimsingi hazigusi maisha ya wengi.
Ni muhimu watendaji wakatanguliza hofu ya Mungu kwanza kabla ya kujinufaisha binafsi na fedha za umma, kwa kuwa wanaowadhulumu ni watu ambao wangeendelea kuishi ikiwa huduma za afya zingeboreshwa kwenye maeneo yao au wangepata elimu na maji kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.
Ikiwa mama, mtoto au Mtanzania anapoteza maisha kwa kuwa tu analazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma hizo zimekosekana kwa sababu kuna mtu ametumia mwanya huo kujipatia fedha za kujinufaisha yeye na familia yake, basi kuna tatizo kubwa na inavunja moyo walipakodi.
Ikiwa kila mmoja atakuwa na hofu ya Mungu na kutambua kuwa amepewa dhamana ya kuwatumikia Watanzania, na kila shilingi ikawa na thamani kwa kutekeleza miradi husika, basi mbele ya haki hatakuwa na deni, lakini ikiwa atatanguliza ubinafsi itakuwa ni kuumiza nchi na kujirundikia dhambi.
Zipo nchi zimefikia kiwango cha juu kabisa cha nidhamu ya utumishi wa umma kwamba mtu anaacha kujifikiria mwenyewe bali anawafikiria wananchi, anapopewa jukumu analitekeleza kwa weledi, ustadi, uadilifu na uaminifu mkubwa kwa kuwa anajua ipo siku ataulizwa au nafsi itamuuma sana kuwa hakuwatendea haki wengine.
Kila mwaka ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inabainisha uwapo wa madudu mengi ambayo yanatokana na usimamizi mbovu wa fedha za umma, na kwa ujumla huonyesha jinsi gani watu wanashindwa kuwajibika, hivyo kusababisha upotevu wa fedha za umma.
Haitarajiwi kuona fedha hizi zinaishia mikononi mwa wajanja wachache bali tuone miradi iliyotekelezwa kwa kiwango cha juu. Tunarajia kuona uzalendo katika kujali Watanzania wengine badala ya ubinafsi wa kujilimbikizia mali.
Fedha hizi na nyingine zinazopokelewa kutoka nje ni mkopo kwa Watanzania ambao watazilipa kwa miaka mingi ijayo, ndiyo maana inatakiwa uaminifu na uwajibikaji wa hali ya juu kuhakikisha zinatekeleza miradi husika.
Ikiwa Watanzania wataendelea kulipa deni hili na mengine lakini wanaona maboresho au miundombinu mizuri ya afya, maji, barabara na elimu, basi maumivu yake siyo makubwa kama ambavyo watalipa deni lakini fedha zimechukuliwa na walafi wachache.
Ni muhimu waliopewa dhamana wakafanye kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu huku wakitambua dhamana kubwa waliyonayo kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania. Watakaofanya vinginevyo Rais Samia asisite kuwawajibisha.










