Mbunge wa Manonga mkoani Tabora, Seif Gulamali (CCM), alitoboa siri hiyo katika mahojiano maalumu na gazeti hili na kubainisha kuwa alikuta karatasi wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini mwa mwaka 2016/17 kwenye meza yake bungeni zikiwa na maelezo ya kutetea vipimo vya vinasaba vya mafuta, ambavyo vilisababisha mjadala mkali bungeni
Gulamali ambaye ni kipindi chake cha kwanza kuwa bungeni, alieleza jinsi alivyoshtukia kuingizwa kwenye kadhia ya rushwa na kutetea vitu bungeni bila kuvijua kiundani.
Wakati wa mjadala wa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, mbunge huyo alidai baadhi ya wabunge walikuwa wamehongwa kuutetea bungeni mfumo huo wa vinasaba unaotumika katika upimaji wa mafuta.
Gulamali alieleza kuwa baadhi ya wabunge wazoefu wamekuwa wakimfuata na kumwambia amepata nafasi hiyo ya kuwakilisha wananchi kwenye chombo hicho katika kipindi kibaya kwa kuwa `pesa za rushwa’ kwa wabunge zimepungua kulinganisha na ilivyokuwa mabunge yaliyopita.
Mbunge huyo anastahili pongezi kwa ujasiri wake wa kufichua jinsi wabunge wetu wanavyoingizwa katika mitego ya rushwa pamoja na kuonyesha kwamba anaichukia rushwa kwa vitendo.
Ni watu wachache katika jamii yetu kama mbunge huyo, ambao wana uzalendo wa kuthubutu kuzungumza hadharani kuhusu baadhi ya watu katika jamii wanavyotumia mbinu mbalimbali kutaka kulitumia Bunge kupitisha mambo ambayo wana maslahi nayo wao binafsi na si kwa manufaa ya taifa.
Bunge kama chombo cha kutunga sheria na kuwasemea wananchi, halipaswi kutumiwa kwa maslahi ya watu binafsi kwa kuwashawishi kwa njia ya rushwa baadhi ya wabunge waunge mkono na kupitisha mambo yao.
Kama alivyosema Gulamali, jukumu la kwanza la wabunge ni kuwakilisha wananchi. Pili, kuisimamia serikali, hivyo mbunge anatakiwa kuisaidia serikali na asipofanya hivyo, maana yake hafanyi kazi yake ipasavyo.
Itakumbukwa pia kuwa wabunge wetu wamekula viapo, hivyo kwa kujiingiza katika rushwa ni kwenda kinyume cha viapo hivyo.
Kwa kuwa mambo hayo yamefichuliwa na mbunge, kuna haja kwa mhimili huo kufuatilia madai hayo na ikibainika kuna wabunge wanahongwa kwa ajili ya kutetea maslahi ya watu binafsi wachukuliwe hatua.
Tunaamini kwamba Bunge letu lina wabunge wengi wazalendo, waadilifu na weledi, hivyo tunawashauri kwamba wawe wajasiri kwa kufichua vitendo vya rushwa na kuonyesha kwa vitendo kwamba wanaichukia rushwa kama alivyofanya Gulamali.
Pia wabunge wetu wajenge utamaduni wa kuzipima hoja zinazowasilishwa bungeni kwanza kuona kama zina maslahi kwa taifa. Kwa kufanya hivyo, wataepukana na uwezekano wa kutumiwa na watu wachache wenye maslahi binafsi.
Tunaamini kuwa wabunge wataifanyia kazi changamoto ya mbunge mwenzao, hivyo kuufanya mhimili huo uendelee kuheshimika kwa umma.
Tunasema hivyo kwa kuwa katika miaka ya karibuni zimekuwapo tuhuma kadhaa dhidi ya baadhi ya wabunge wanaodaiwa kuomba rushwa na kupokea rushwa kwa kutumia nafasi zao; hivyo kuutia doa mhimili huo.










