Hili tumelishuhudia na kudhihirisha umuhimu wao katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19, ambapo serikali na nchi mbalimbali zilisitisha mashabiki kuhudhuria viwanjani.
Katazo hilo mbali na kuzikosesha timu na wanamichezo mapato ya kujiendesha, lakini lilipunguza shangwe kwa mashindano mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea mpaka mabingwa walipopatikana na hatimaye kujifunza kitu kipya.
Ilionekana wazi kukosekana mashabiki hao viwanjani kulipunguza ushindani kwa baadhi ya mechi kwa sababu wachezaji wake walikosa watu wa kuwahamasisha na kucheza katika viwango vya juu kama walivyozoeleka.
Lakini mashabiki hao ambao ni sawa na mchezaji wa 12 katika timu kama wanavyoitwa kwenye upande wa mchezo wa soka, bado wanatakiwa kufahamu mipaka na hazi walizonazo wanapokuwa kwenye viwanja kwa ajili ya kuzishabikia au kuziunga mkono klabu wanazozipenda.
Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia mashabiki wakivuka mipaka kwa kuingilia majukumu ya makocha au ya viongozi wanaoongoza klabu au vyama vya mikoa kwa sababu tu mambo hayaendi kama walivyotarajia.
Tunapenda kuwakumbusha pamoja na umuhimu wao, lakini ni vyema mashabiki wakafahamu mipaka yao na kujiepusha kuziingiza timu au wanamichezo wanaowashangilia kwenye wakati mgumu wa kufungiwa au kutozwa faini.
Katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Gwambina FC dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba kutoka jijini Dar es Salaam kulionekana vitendo vya mashabiki kumrushia shupa mwamuzi msaidizi namba moja kwa ishara ya kutokubaliana na uamuzi aliofanya wa kukataa bao lililofungwa na mchezaji wao, Joash Onyango.
Kwa kufanya hivyo, mashabiki hao wanaiweka timu yao kwenye hatari ya kutozwa faini au adhabu nyingine kubwa, hali ya kuwa walipaswa kutulia na kuacha viongozi wao kuchukua njia sahihi ya kuwasilisha malalamiko yao katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa sababu kitendo cha kumpiga mwamuzi au waamuzi hakiwezi kubadilisha matokeo.
Katika dunia hii ya utandawazi ambapo mechi zote za Ligi Kuu Tanzania Bara zinaonyeshwa mubashara, idadi kubwa ya matukio yanayofanyika uwanjani huonekana kupitia kamera zilizoko kwenye viwanja hivyo, na kwa sababu hiyo huu ni wakati wa mashabiki kujirekebisha au kuacha kabisa kujichukulia hatua mkononi.
Vurugu au fujo hizo za viwanjani unaweza ukaziangalia katika ngazi ya Ligi Kuu, lakini kumbe wasimamizi wa mchezo huo wakubwa katika ngazi ya CAF au FIFA wanaweza kuchukua picha hizo za vurugu na hatimaye kuinyima Tanzania haki ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya kimataifa pale itakapoomba kwa ushahidi kwamba nchi hii si salama.
Nipashe inawasisitisha mashabiki, viongozi na wachezaji kuimarisha nidhamu wanapokuwa uwanjani kwa ajili ya kuiongezea heshima na thamani Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo msimu huu imetoa timu moja iliyoingia katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa mashabiki wa Simba, wao ndio wanatakiwa kuongeza utulivu kwa sababu wapinzani wa timu yao (timu nyingine saba zilizotinga robo fainali), kwa sasa wanawafuatilia wawakilishi hao kwenye kila mchezo wanaocheza ili kuwapeleleza kwa ajili ya kukabiliana nao kwenye hatua hiyo inayofuata.
Tunawakumbusha katazo la kutocheza na mashabiki lilivyopunguza shamrashamra katika baadhi ya michezo kwenye msimu uliopita na huu, hivyo tukumbuke utulivu wa mashabiki huisaidia timu wanayoishangilia kuvuna matokeo chanya na si kujiweka kwenye mazingira ya kuadhibiwa.










