Wapo wabunge waliosema kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo kuna wananchi wanakunywa maji machafu ambayo hayastahili kunywewa na binadamu, lakini ni kutokana na ukosefu wa huduma hiyo.
Baadhi walikwenda mbali zaidi ya kushika Shilingi kwa madai kuwa upotevu wa maji unaongezeka kiasi cha kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 332, na kutaka hatua mahususi, ikiwamo kuunda kikosi kazi cha kufuatilia na kuja na suluhisho la kudumu.
Wabunge walisema hali ni mbaya zaidi vijijini kwa kuwa hakuna majisafi na salama na kwamba ule mpango wa kumtua ndoo mama bado haujafanikiwa kwa kuwa wanahangaika kutafuta maji.
Serikali inasema kwa sasa upatikanaji wa maji kwa mijini ni asilimia 80 na vijijini ni 73.2, lakini baadhi ya wabunge walionyesha wasiwasi wao kuhusu takwimu hizo kwa kuwa bado huduma ya maji ni changamoto kubwa.
Aidha, alisema fedha za miradi ya maji ni nyingi, lakini bado huduma hiyo haipatikani inavyotakiwa, huku hata maeneo ya mijini kukiwa na tatizo licha ya jitihada nyingi zilizofanyika.
Serikali imeahidi marekebisho makubwa kuhakikisha maji yanapatikana ikiwamo kusimamia kwa karibu miradi yote ya kutoa maji kwenye mito na ziwa kwa ajili ya kuyafikisha kwenye makazi ya watu.
Katika kukabiliana na uhaba huo serikali imeahidi kutekeleza miradi 1,527 ya maji katika maeneo ya vijijini na 114 maeneo ya mijini ikihusisha upanuzi na ukarabati wa miundombinu.
Pia serikali itachimba visima 516, kujenga mabwawa 33 hususani maeneo kame.
Ni hatua nzuri katika kujibu kilio cha wabunge, lakini bado inatakiwa kuwa na usimamizi wa karibu ili kuhakikisha miradi hiyo sio hewa bali yenye tija kubwa ya kuleta mabadiliko makubwa kwa wananchi.
Ni muhimu thamani ya fedha ikaonekana na kudhibiti mianya yote ya ubadhirifu ambayo ndiyo mchwa anayetafuna sekta ya maji nchini.
Kilio cha maji kimekuwa kikubwa na lengo la kumwezesha mwananchi kupata maji umbali usiozidi mita 400 inashindikana na sababu kubwa ni miradi mingi kutotoa maji kama inavyotakiwa.
Na katika kuonyesha kuwa kilio ni kikubwa Rais Samia Suluhu Hassan, alimtaka Waziri wa Maji kuongeza kasi ya usimamizi na huku akitumia usemi wa kiongozi huyo ‘Ukinizingua nakuzingua’ na kwamba ni vyema akawajibika mapema kabla hatua hazijachukuliwa.
Kwa msingi huo ni muhimu kuhakikisha huduma za maji zinapatikana ipasavyo, nia ya kumtua mama maji ionekane, kwani inashangaza hadi sasa upatikanaji wa maji hata kwa miji na majiji yenye vyanzo kuna changamoto kubwa ya huduma hiyo.
Hakuna ubishi kuwa maji yanahusiana moja kwa moja na suala la afya na iwapo maji yatapatikana kwa wakati maana yake maambukizi ya mgonjwa mengi yatadhibitiwa.
Lakini pamoja na jitihada hizo ni muhimu sana kasi ya kuelimisha wananchi ikaongezeka kwa kutumia maji kwa usahihi ili kuwezesha watumiaji wengine kupata huduma hiyo kwa uhakika zaidi.
Wapo wananchi bila uelewa wanatumia maji ya bomba ambayo yanaandaliwa kwa gharama kubwa kumwagilia bustani za maua, mboga na wengine kufyatulia matofali, wafuatiliwe na kuelimishwa umuhimu wa kuvuna maji ya mvua kwa kazi hiyo.










