Wakati akitoa wito huo, Mwenyekiti wa JUVI-CUF, Hamidu Bobali, alisema msimamo wa chama kikuu cha upinzani hicho Zanzibar ni kutoshiriki uchaguzi huo kwa sababu wanachotambua ni kuwa Maalim Seif Sharif Hamad alishashinda katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Wawakilishi uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Kauli ya Bobali si mpya katika kuelezea msimamo huo wa upande mmoja wa demokrasia teketeke ya Zanzibar, lakini ni ya mwishoni zaidi katika muendelezo wa miito ya kususia uchaguzi wa leo wa marudio kutoka CUF.
Kama ambavyo tumesema, Nipashe, kauli ya Bobali si mpya katika kuelezea msimamo huo wa upande mmoja wa demokrasia teketeke ya Zanzibar.
Lakini tunalazimika kuizungumzia leo, Nipashe, kwa sababu Bobali alikwenda mbali zaidi mara mbili:
Kwanza, alisema Bobali, JUVI-CUF inalaani vitendo vinavyofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya vijana wa CUF ambao wamekuwa wakipigwa na kuteswa bila sababu za msingi, jambo ambalo ni ukiukwaji wa Katiba na haki za binadamu.
Lakini pia, alisema Bobali, kwamba kama wapinzani wanasikitishwa na kauli aliyoitoa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Sadifa Juma (MB), kupitia ukurasa wake katika mtandao wa Facebook, wa kuwataka vijana wa CCM wajibu mapigo kwa kuwapiga vijana wa CUF.
Kauli hii imetushitua Nipashe si kwa sababu ina kila dalili ya kuchochea kuendelea kuwapo kwa uvunjifu wa amani, lakini zaidi kwa sababu kama misimamo hiyo ya jumuiya za vijana itaendelea, hapatakuwa na amani Zanzibar kwa angalau kizazi kimoja zaidi kutokana na uhasama huo kujengeka miongoni mwa taifa la kesho.
Ni siri iliyo wazi kuwa umoja wa Wazanzibari na amani iliyokusudiwa kuendana nao katika kizazi cha sasa ni vya kulegalega.
Na ni katika kuweka sawa hilo, basi, ililazimika kufanyika kwa marekebisho ya katiba juu ya muundo wa utawala yaliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ambayo itakuwa katika nafasi ndogo ya kuendelea kuwapo iwapo CUF haitoshiriki uchaguzi huo kama ilivyo msimamo.
Ndiyo maana, basi, tunachukua nafasi hii Nipashe kushauri Wazanzibari wote kuchukulia uchaguzi wa marudio wa leo Jumapili kama mwanzo wa mchakato wa kurejesha umoja na amani ya Zanzibar na si tukio la kupata mshindi kati ya CCM na CUF.










