Inaelezwa kuwa Mahakama ya Mkoa wa Wete imefutilia mbali shtaka la mtoto wa miaka 16 kumnajisi mwenzake mwenye miaka mitano, baada ya mashahidi kukataa kufika mahakamani.
Taarifa zinaeleza kuwa aliyenajisiwa ni mtoto mdogo wa kiume na kwamba shauri hilo lipo muda mrefu mahakamani bila ya kusikilizwa kwa vile mashahidi hawaonekani.
Si nia yetu kurejea kilichotokea mahakamani, lakini tunashauri serikali na wadau wa haki za watoto na sheria kutizama upya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana na ile ya Watoto ya mwaka 2009, Kanuni ya Adhabu na mwenendo mzima wa kesi hizo.
Suala la kukaidi kufika mahakamani hasa kwenye mashauri ya kunyanyasa watoto kijinsia na kingono , ubakaji wa wanawake na mimba kwa watoto na wanafunzi limekuwa likipigwa mpira na mara nyingi mashtaka kufutwa.
Kuna maelezo kuwa wazazi, walezi , watuhumiwa na jamaa zao wanalindana ili kupoteza ushahidi na kuzima kesi hizo.
Sote tunasikia kuwa walalamikaji wanalipwa na suala linamalizwa nje ya mahakama. Mathalani, binti akipata ujauzito analalamika polisi na kuonyesha ushirikiano, lakini inapotokea aliyembaka anaahidi kuwalipa wazazi au walezi na kumtunza, anakana kila kitu kizimbani.
Inakuwa ni njia rahisi ya kukwepa mkono wa sheria kwa wanaobaka watoto, wanaonajisi na wanaofanya kila aina ya uhalifu dhidi yao kwa vile hakuna ushahidi. Inarahisisha kazi kwa mwendesha mashtaka ambaye anafuta kesi.
Tunaomba serikali ya Zanzibar pamoja na ya Muungano zitazame upya mazoea haya ya kuikwepa sheria kwa sababu yoyote inawaumiza watoto, wanawake na wanyonge na kuongeza uhalifu kwenye jamii.
Mapitio ya sheria yafanyike ili kuwakamata na kuwahukumu wazazi, walezi na jamaa wengine ambao ndugu zao watahusika kwenye kulinda wahalifu wanaonajisi au kudhulumu watoto kingono.
Sheria pamoja na kuharamisha matendo hayo pia itamke wazi jinsi ya kukabiliana na kesi hizo hasa pale mashahidi wanapokataa kufika mahakamani au walalamikaji wanapokataa kushirikiana na mahakama.
Licha ya kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeingia kwenye kesi hizo za mimba utotoni na hata nyingine zinazohusiana na masuala ya kujamiiana, ni vyema pia sheria ya TAKUKURU ikarekebishwa ili ihusike moja kwa moja kuwabana wazazi, walezi na jamaa wanaoshirikiana kuzuia ushahidi mahakamani.
Tukumbuke wahalifu wakiachwa kunajisi, kuwapa ujauzito na hata kuwaambukiza maradhi watoto bila mienendo hiyo kukomeshwa ni hatari kwa taifa letu ambalo pamoja na kuwa na raia wahalifu tutakuwa pia limelea na kupalilia mienendo ya mmomonyoko wa maadili.
Tunaziomba serikali zichukue hatua kwa sababu kesi nyingi za makosa ya kujamiiana hazisikilizwi katika mahakama zetu kwa sababu ya kukosekana ushahidi na sasa ni mazoea.
Ni wazi kuwa haya ni mambo yanayotokea kote Bara na Visiwani na huenda vijijini mambo yakawa magumu zaidi kwa vile hata kiwango cha uhamasishaji ni kidogo.
Tunasikitika kuwa washtakiwa hawaadhibiwi, huku matendo hayo yakiongezeka kwenye jamii, mahakama zinapuuzwa hata zinapowapa hati ya kuitwa shaurini kama mashahidi hawatokea tena bila kuwa na sababu za msingi. Ndiyo maana tunaomba serikali zichukue hatua kunusuru taifa letu.










