Tuitumie vizuri fursa iliyoletwa na Ufaransa

22Oct 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tuitumie vizuri fursa iliyoletwa na Ufaransa

HIVI karibuni Waziri wa Mambo ya Nje, Biashara na Vivutio vya Kiuchumi wa Ufaransa, Franck Reister, alikuja nchini na ndege ya Shirika la Air France ya moja kwa moja kutoka Paris, Ufaransa hadi Zanzibar.

Ujio wake huo uliambatana na uzinduzi wa rasmi wa safari za ndege za shirika hilo za Ufaransa-Zanzibar, viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakishiriki.

Waziri huyo pia alizuru Dar es Salaam katika Ubalozi wa Ufaransa nchini na kuona magari yanayotengenezwa na kampuni moja kutoka nchini humo ambayo yana mfumo wa umeme, yakielezwa kuwa ni rafiki kwa mazingira kwa kuwa hayana kelele na hayatoi hewa ukaa ambayo huchangia mabadiliko ya tabianchi.

Tayari Kampuni ya Utalii ya Mount Kilimanjaro Safari Club inatumia magari hayo kusafirisha watalii, magari hayo yakitengenezwa kwa ushirikiano kati ya kampuni ya Ufaransa na Tanzania, huku kukiwa na ushirikishwaji wa teknolojia.

Waziri huyo pia alikutana na mawaziri wanne wa sekta za uwekezaji, nishati, usafirishaji na mambo ya nje pamoja na kampuni ya Kifaransa nchini na wafanyabiashara mbalimbali kujadili namna ya kuendelea kushirikiana kwa manufaa ya nchi zote.

Kiongozi huyo wa Ufaransa pia alikutana kwa mazungumzo na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, yote ikiwa ni namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ambazo kwa miaka mingi zimekuwa na uhusiano wa kidiplomasia.

Viongozi hao wakashiriki uzinduzi wa duka la kisasa la bidhaa mbalimbali kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal Three, ambayo yanamilikiwa na kampuni za Ufaransa na Tanzania, ambayo yametoa ajira kwa Watanzania.

Kuanza upya kwa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Paris, Ufaransa hadi Tanzania ni hatua kubwa katika sekta ya utalii kwa kuwa mara ya mwisho ndege hiyo kuja nchini ilikuwa mwaka 1974, yaani miaka 47 iliyopita.

Ndege hizo za Ufaransa zinabeba mamia ya wageni kutoka nchi za Ulaya na kwingineko duniani ambao huja nchini kwa sababu za kikazi au kitalii. 

Nipashe tunaamini ushirikiano huo utanufaisha pande zote, kwamba wakati kampuni za Ufaransa zikija kuwekeza nchini, Watanzania waone fursa za uwekezaji kwenye nchi hiyo au kujifunza ubunifu na teknolojia katika kuleta mabadiliko kwao.

Hakuna ubishi Ufaransa ni moja ya nchi zilizoendelea si tu kiteknolojia, bali pia kiuchumi duniani, yapo mengi ya Tanzania itajifunza kutoka taifa hilo la Bara la Ulaya kwa kadri ya maudhui na mahitaji ya nchi, lakini kulinda mila na tamaduni kusije kusahaulika.

Tunaamini ushirikiano huo ni fursa ya ajira katika sekta mbalimbali ikiwamo utalii kwa kuwa ujio wa watalii kwa wingi nchini unapaswa kwenda sambamba na kuzalisha rasilimali watu ya kuitumikia sekta ya utalii, hivyo Watanzania wengi watapa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Tayari viongozi wa serikali wameihakikishia nchi hiyo kuwa vikwazo vilivyokuwapo vimeondolewa na sasa ni wakati wa kampuni za nchi hizo kushirikiana, huku kila upande ukiahidi ushirikiano thabiti. 

Ni muhimu vikwazo vyote kwa pande zote vikaondolewa ili kuhakikisha fursa zilizopo zinaendelezwa kwa ajili ya kunufaisha wengi, hasa Tanzania -- kwamba sasa tuone Watanzania wakipewa kipaumbele cha ajira na kupata ujuzi kutoka kwa wageni wanaokuja kuwekeza nchini. 

Ni wajibu wa serikali kwa kushirikiana na taasisi zake na sekta binafsi kuwa na mkutano wa pamoja kujadili kwa kina ushirikiano huo sambamba na kuwajengea uwezo wananchi namna ya kuziona fursa mbalimbali za nje ya nchi kwa manufaa yao binafsi na taifa kwa ujumla.

Tunatarajia kuona kumiminika kwa kampuni za nchi hiyo kuwekeza nchini kunakwenda kuwanufaisha wananchi wengi, badala ya maslahi ya mtu mmoja.

Miaka kadhaa iliyopita kulishuhudiwa namna baadhi ya viongozi ambao pasi na kuangalia maslahi mapana ya nchi, waliingia mikataba mibovu ambayo mwisho wa siku Watanzania wamebeba mzigo mkubwa wa hasara. 

Nipashe tunaamini ni aibu nchi kuwa na raslimali na utajiri mwingi lakini raia wake hawaoni umuhimu wake kwa kuwa tu kuna viongozi waliingia mikataba ambayo haikuzingatia maslahi mapana ya nchi.

Ni katika muktadha huo, Nipashe tunaona kuna haja Tanzania kuchangamkia fursa iliyoletwa na Ufaransa nchini wakati huo wakiwa na hadhari katika uamuzi wowote unaogusa maslahi ya Watanzania.