Tuangalie mafuta hayo yana viwango?

20Apr 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tuangalie mafuta hayo yana viwango?

SUALA la mafuta ya kula kuwa changamoto kila wakati limeanza kuwa kama jambo la mazoea. Kama ambavyo sukari nayo inafika kipindi ikaondoka sokoni kwa maelezo kuwa wazalishaji wanasafisha vikaango, vivyo hivyo mafuta nayo yanapotea.

Kuna maelezo kuwa miwa ikishakamuliwa ‘juisi’ yake inapitishwa katika mitambo ya kuikausha ili iwe kama ‘mchanga’ ambayo ndiyo sukari na eneo inapokaushiwa huitwa kikaango.

Changamoto ya sukari kuadimika kama yalivyo sasa mafuta imekuwa ni suala la mara kwa mara na kinachotokea kwenye upungufu huo ni maduka kuongeza bei na sasa ndicho kinachotokea kwenye mafuta.

Hata hivyo, kinachotusukuma leo ni kuzungumzia mafuta. Kwa muda mrefu suala la mafuta halijaeleweka kwa vile sokoni kuna aina ya mafuta ya kula ‘isiyoeleweka’ au ya viwango duni.

Mafuta hayo ndiyo yanayotumiwa na wapishi wa aina mbalimbali iwe migahawani, mama na babalishe na kukaanga vitafunio mbalimbali kama mihogo, chips , ndizi na vyakula vingine vingi.

Yapo kwenye ndoo kubwa na ndogo na hata madumu ambayo wateja hupimiwa kwenye vipimo vidogo au lita moja wanaponunua rejareja lakini ukiyaangalia ni kama hayana viwango. Yanaelekea kana kwamba hayayeyuki. Yana masimbi Tena yameganda.

Haya ndiyo mafuta yanayotumiwa karibu kila mahali kukaanga chapatti na vitafunwa mbalimbali na ndiyo yanayotumika kupikia vyakula kwenye migahawa na sehemu kubwa mijini na vijijini.

Ukifuatilia unakuta kuwa hayayeyuki kikamilifu na pengine hayana kiwango yakilinganishwa na mengine yanayoelezwa kuwa yamechunjwa mara kadhaa na kemikali ambazo pengine zina madhara kwa binadamu.

Mafuta yanayouzwa ghali ni yale ambayo yamechujwa na kusafishwa yakawa meupe na ndiyo ambayo huuzwa ghali zaidi na ndiyo yaliyoelezwa kuwa yameadimika.

Mafuta hayo tunafikiri wakati umefika wa kuyachunguza, tukishauri Shirika la Viwango pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba kutoa maelezo kuhusu ubora na viwango vyake kwa afya ya walaji.

Mafuta hayo yanauzwa kwa wingi kwenye chupa za plastiki yakijazwa kwenye chupa hizo zinazookotwa mitaani baada ya watu kuzitupa wakishamaliza kunywa maji.

Uuuzaji mafuta hayo yaliyojaa sokoni, madukani, mnadani na kwenye maeneo ya biashara za vyakula, unatia mashaka.

Na hofu yetu ni kwamba huenda hayako salama kiafya kutokana na ukweli kuwa yanaganda, yana masimbi na rangi si angavu.

Licha ya maelezo kuwa kuna shehena ya mafuta ya meli iliyotoa nchini, bei za mafuta hasa ya viwango vya juu au yaliyochunjwa ‘double refined’ yanayotumiwa na wachache bei zake zimeendelea kupaa. Lita moja ikiuzwa Sh. 8,000 kwa jumla na takribani 10,000 kwa rejareja.

Ukweli ni kwamba mafuta yanayotumiwa mitaani kukaanga vyakula kuanzia samaki hadi vitumbua yanaibua maswali mengi na mara nyingi huwa hayaadimiki, wala bei zake hazibadiliki mara kwa mara.

Tunapendekeza mafuta hayo kuchunguzwa kwa sababu si wafanyabiashara wote wanaotoa taarifa za ukweli huenda wapo wadanganyifu na mara nyingi wanakwepa kuuza bidhaa hiyo kwa utaratibu unaofahamika na badala yake huwapa wamachinga wawasaidie kuuza.

Watu wengi hasa familia za uchumi wa kati hawatumii mafuta hayo , lakini kwa vile ni wateja wa migahawani na wa chips zinazouzwa mitaani huenda nao wanakula mafuta hayo wanayoyakimbia.

Nia yetu ni njema na tunaamini kuwa iwapo ukweli utafahamika kuhusu mafuta hayo ukweli ukifahamika kama hakuna ubora bidhaa hizo zinaweza kuondolewa sokoni kama ikibainika kuwa hazina viwango.