Tahadhari dhidi ya corona muhimu

07May 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tahadhari dhidi ya corona muhimu

TAARIFA mbalimbali duniani zinaeleza kuwa aina mpya ya kirusi cha COVID kimeibuka nchini India, na tayari mamia ya wananchi wamefariki, huku hospitali kuzidiwa na wagonjwa na huduma ya hewa safi ikikosekana.

Habari katika vyombo vya habari vya kimataifa zinaonyesha jinsi nchi hiyo inavyohangaika kukabiliana na mlipuko huo, huku wananchi wakionekana wakichoma miili ya ndugu zao kama utaratibu wao wa mazishi, ikwamo kuwapo kwa katazo la kusafirisha miili ili kuepuka kusambaa kwa ugonjwa huo.

Tanzania siyo kisiwa kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan, amesema wakati akiwaapisha makatibu wakuu, na ndiyo maana aliunda kamati maalum ya wataalamu kufanya uchunguzi ili kujua namna Tanzania itakavyo likabili suala hilo.

Tayari tunaona serikali imeimarisha ukaguzi, upimaji na ulinzi katika viwanja vya ndege na mipakani huku hofu kubwa ikiwa ni uhusiano baina ya Tanzania na India na uwapo wa safari za ndege kutoka na kuja nchini.

Tayari Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), limesitisha safari za India, hadi hapo hali itakapotengamaa nchini humo.

Machi, mwaka jana, kwa mara ya kwanza Tanzania ilirekodi kisa cha kwanza cha mgonjwa wa corona, na hali ilitulia baadaye, na mwaka huu Februari hadi Machi ilijirudia tena, na serikali ilieleza kuwa kuna changamoto ya upumuaji na wananchi kutakiwa kutumia dawa za asili ikiwamo kujifukiza.

Kwa kuwa Tanzania siyo kisiwa tunaona ni muhimu kujipanga kwa kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari za kujikinga ikiwamo uvaaji barakoa, kunawa mikono na kuepuka misongamano kwa kuacha safari zisizo za lazima.

Ni muhimu pia huduma za afya zikaimarishwa na kuhakikisha zinapatikana ikiwamo mahitaji yote ya msingi ya kukabiliana na corona, ili kuepusha madhara kuwa makubwa kwa kujipanga vyema kukabiliana na hali.

Tanzania inapakana na nchi za Kenya, Uganda, Congo, Burundi, Rwanda Msumbiji, Malawi na Zambia na kote huko shughuli za kiuchumi za watu kuingia na kutoka nchini zinazoendelea, kwenye mipaka hiyo kuna uwezekano wa ugonjwa huo kuingia nchini.

Ni muhimu elimu kwa umma ikaanza mapema, na kama Rais Samia alivyotaka kila mmoja kujilinda, basi jitihada zifanyike kuanzia ngazi ya mtaa hadi mkoa, kuhamasisha wananchi kujilinda ili kupuka uwezekano wa kusambaa kwa ugonjwa huo ikiwa utaingia nchini.

Tayari Chama cha Madaktari Tanzania (MATI), kimetoa angalizo kwa serikali kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa baadhi ya watu vipimo vyao kuonyesha kuwa hawana ugonjwa huo wakati wana dalili zote.

Kwa hali hiyo, hata kazi ya kupima kabla na baada ya kuingia nchini inaweza isisaidie sana kwa kuwa kirusi kinaweza kisionekane, ni muhimu kama nchi kujikinga na kuepuka uwezekano wa kutokea maangamizi.

Hakuna ubishi kuwa corona ni hatari na India imeelemewa, zipo nchi zimepoteza wapendwa wao wengi, lakini zipo ambazo hazijarekodi kisa chochote kutokana na kuchukua tahadhari zote muhimu ikiwamo kuvaa barakoa, kuepuka misongamano, kunawa mikono mara kwa mara.

Suala la afya ni la mtu binafsi, ni muhimu jitihada za kujikinga zikafanywa na mtu binafsi ili kuepuka kupotea kwa nguvu kazi.