Sheria ya uchaguzi muhimu iboreshwe

25Aug 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Sheria ya uchaguzi muhimu iboreshwe

MWISHONI mwa wiki, Rais Samia Suluhu Hassan, alipokea Ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 iliyowasilishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), alisema inatakiwa kuangalia upya sheria ili zisitumike kuwanyima watu haki wakati wa uchaguzi.

Haki hizo ni kukosea au makosa mengine kwenye fomu za kuomba kuteuliwa kugombea, kauli ambayo lilipigiwa makofi na washiriki wa mkutano, ambao wengi walikuwa kutoka vyama vilivyoshiriki uchaguzi mkuu mwaka jana.

Tunampongeza Rais Samia kwa kuliona hilo na iwapo sheria hizo zitafumuliwa, ni vyema ushiriki wa wadau wote ukawapo, ili kuondoa malalamiko katika kujenga demokrasia nchini. Yapo mengi yanayolalamikiwa kwenye uchaguzi kila unapofanyika, na mwisho wengi huishia kuona kuwa ili mchakato huo usiwe na malalamiko, ni muhimu kuwa na Katiba mpya.

Mwaka 2014, Bunge Maalum la katiba lilikamilisha mchakato wa Katiba mpya ambao ulianzia kwenye ukusanyaji wa maoni ya wananchi na kupata rasimu chini ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Katiba inayopendekezwa ilipaswa kwenda kwenye hatua ya mwisho ya kurudishwa kwa wananchi kwa ajili ya kura ya maoni, lakini haukufika mwisho hasa baada ya kuwapo mvutano kati ya wajumbe ulioonekana kusababishwa na tofauti itikadi za vyama.

Baada ya mchakato huo kukwama kulikuwa na ahadi ya kufanya marekebisho ya katiba iliyopo ya mwaka 1977 ili kuweka mazingira bora ya uchaguzi mkuu wa 2015.

Mambo yaliyotakiwa kufanyiwa marekebisho kwenye Katiba ya sasa ni kuruhusu kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi, kuwaruhusu wagombea binafsi, kuruhusu matokeo ya uchaguzi wa rais kupingwa mahakamani na anayeshinda urais kutakiwa kupata kura zaidi ya asilimia 50.

Kata hivyo, serikali ya Jakaya Kikwete haikuitekeleza ahadi hiyo. Rais aliyemfuatia, Hayati John Magufuli, alisema suala la katiba mpya halikuwa ajenda yake kwa wakati huo, lakini Rais Samia ameahidi kulishughulikia, ingawa ameomba apewe muda kwanza aisimamishe nchi.

Vyama vya upinzani na wadau wengine wameendelea kupaza sauti kudai Katiba mpya, kutokana katiba ya sasa hasa Sheria ya Uchaguzi kuonekana ni kikwazo kikubwa kwenye mchakato wa uchaguzi.

Kwa mfano, Zambia iliyofanya uchaguzi Agosti 12, mwaka huu, imeonyesha kwamba kuwapo kwa mazingira mazuri ikiwamo katiba na sheria nzuri ndiyo dawa ya kutokuwapo malalamiko na uchaguzi kuwa huru na haki pamoja na kuaminika.

Sheria yao imeruhusu mgombea binafsi na wapo ambao walishindwa kwenye kura za maoni ndani ya vyama vyao na na kuendelea na ndoto zao za uongozi wa kisiasa kama wagombea binafsi.

Lakini inaruhusu mchakato wa kupata makamishna wa tume ya uchaguzi ambao ni wa wazi na hauingiliwi na yeyote kiasi kwamba hata ikitangaza matokeo yanaaminika.

Pia, Katiba yao inataka mshindi kuwa na kura zaidi ya asilimia 50 na sheria inaruhusiwa matokeo ya rais kupingwa mahakamani baada ya tume kuyatangaza. Mahakama inaweza kuamuru kura kurudiwa kuhesabiwa au kufuta uchaguzi kutegemea na ushahidi.

Ni muhimu maoni ya wadau wa uchaguzi kusikilizwa na kushughulikia kasoro zote ambazo zinazua shaka ya mchakato hadi kutangazwa kwa mshindi. Tunatarajia kuona viongozi wetu wanayachukua na kuyafanyia kazi mazuri yote yalioonekana katika uchaguzi wa Zambia ili nchi yetu iwe na uchaguzi mzuri, huru na haki pamoja na kuaminiwa na wadau wa uchaguzi nje na ndani ya Tanzania.