Serikali ijipange kwa ongezeko wanafunzi

23Apr 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali ijipange kwa ongezeko wanafunzi

TOLEO letu la jana nilikuwa na ripoti iliyoangazia kasi ya ongezeko la wanafunzi iliyochagizwa na kuanza kutekelezwa kwa Mpango wa Utoaji wa Elimumsingi Bila Malipo, maarufu elimu bure.

Tathmini na ripoti mbalimbali za kiukaguzi zikiwamo za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zinaonyesha kuwa mwakani kutakuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliodahiliwa kujiunga darasa la kwanza kwa mpango wa elimu bure watakaojiunga na kidato cha kwanza.

CAG ameshanyooshea kidole suala hilo, akiitaka serikali kujipanga kukabiliana na 'mliopuko' huo ambao maandalizi yake ya kina yanapaswa kufanyika ndani ya miezi minane iliyobaki.

Mkaguzi Mkuu huyo ameshabainisha kwamba udahili wa wanafunzi katika shule za msingi nchini uliongezeka kutoka wanafunzi milioni 4.8 mwaka 2001 hadi milioni 8.34 mwaka 2016, yaani katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mpango wa elimu bure.

Katika miaka hiyo minne iliyopita, mkaguzi hiyo wa kitaifa aliainisha idadi ya wanafunzi kwenye shule za msingi nchini ilikuwa milioni 8.34 kwa shule za serikali na madarasa yao yalikuwa 108,448, ambayo ni wastani wa nusu (asilimia 52) ya mahitaji halisi ambayo ni madarasa 208,540.

Pia, kwa kutumia kigezo hicho, inamaanisha kulikuwa na ukiukwaji wa kanuni za ufundishaji bora, unaohitaji darasa liwe na wanafunzi wasiozidi 45, lakini kulinganisha na hali ilivyokuwa, darasa moja lilisheheni wanafunzi 77, ambayo inakaribia kuwa sawa na madarasa mawili.

Kwa mantiki hiyo, wakati mwaka 2016 kulivyoshuhudiwa mlipuko wa udahili ambao ulielemea uhalisia wa mahitaji kutokana na serikali kuanza kudahili pasipo malipo (elimu bure), tayari miaka kadhaa kabla, jahazi hilo lilikuwa limeanza kuelemewa.

Ndani ya mtazamo wa ubashiri kama wa CAG, tathmini iliyofanywa na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na kongani ya elimu, zinaonyesha katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2024, idadi ya wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza itaongezeka hadi kufikia wanafunzi 1,882,500, ikiwa ni takriban mara mbili ya takwimu za mwaka 2015.

Nipashe tunaishauri serikali kuhakikisha ongezeko hilo la wanafunzi liende sambamba na mahitaji ya madarasa, walimu, vitabu, vyoo na ruzuku ya elimu bure.

Tathmini za kitaalamu kuhusu kasi ya ongezeko hilo zinaonyesha kuwa kutokana na idadi hiyo ya wanafunzi, kutahitajika madarasa 41,833, sasa kukiripotiwa kuwapo uhaba wa madarasa 4,647 katika shule za sekondari nchini, hivyo kufanya uhitaji uwe mkubwa zaidi kufikia madarasa 46,480.

Nipashe pia tunaishauri serikali kujipanga kuongeza matundu ya vyoo 75,000 yatayohitajika, vitabu milioni 18.825, walimu 41,833 na Sh. bilioni 47 kila mwezi kwa ajili ya ruzuku ya elimu bure.

Tunaamini kuwa, bila kuwapo mkakati kitaifa kukabiliana kasi ya ongezeko la wanafunzi iliyopo, CAG akibainisha kuwapo ongezeko la asilimia tano kwa mwaka, wanafunzi wengi walioanza darasa la kwanza mwaka 2016, hawatapata nafasi kujiunga na kidato cha kwanza mwakani kutokana na uhaba wa miundombinu.

Shime, serikali ichukue hatua kukabiliana na ongezeko hili kwa kuboresha miundombinu ya shule iliyopo, kujenga shule mpya na kuajiri walimu wapya ili kukidhi mahitaji.