Serikali ifanyie kazi upungufu wa dawa

14May 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali ifanyie kazi upungufu wa dawa

MJADALA wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, umetawaliwa na kilio kikubwa cha ukosefu wa dawa kwa wananchi, jambo ambalo limeharakisha vifo vya wengi.

Aidha, ukosefu wa huduma bure za afya kwa wazee, wajawazito na watoto ni kilio kingine kilichozungumzwa na kila mbunge aliyechangia mjadala huo wa mwaka wa fedha 2021/22.

Watunga sheria hao walitaka hatua madhubuti kuhakikisha dawa zinapatikana kwa kuwa wananchi wanateseka na hata kwenye Bima ya Taifa ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (ICHF).

Walisema ukosefu wa dawa badala ya kuwa msaada kwa wanachi kwamba waokoe maisha yao, lakini hali imezidi kuwa mbaya, kwa kuwa dawa hakuna na mwisho wengi wanakufa.

Walitoa mfano wa mtu mwenye bima kuandikiwa dawa anapokwenda kwenye dirisha hapati dawa yoyote na kutakiwa kusafiri umbali mrefu kupata dawa kwenye maduka rasmi yanayopokea bima jambo linalomfanya kutumia gharama kubwa na wakifika kwenye maduka wanakosa dawa husika.

Walitaka serikali kuliangalia suala hilo kwa kuwa afya za watu ni muhimu sana, vinginevyo itakuwa ni kupoteza nguvu kazi ambayo inatengenezwa kwa gharama kubwa.

Aidha, walisema kuna watu wanalazwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), lakini bado hakuna dawa, jambo ambalo ni tishio kwa afya endelevu na nguvu kazi ya taifa.

Kilio dhidi ya huduma duni za dirisha maalum la kuhudumia wazee ni kilio cha muda mrefu, ambacho hata kwenye mkutano wa Rais Samia Suluhu Hassan na wazee wa Dar es Salaam kiiibuka na aliahidi mkakati madhubuti kuhakikisha huduma na upatikanaji wa dawa kwa kundi hilo.

Pia kundi la wajawazito kutozwa fedha huku mbunge mmoja akieleza ipo hospitali akizaliwa mtoto wa kiume ni Sh. 50,000 na wa kike ni Sh. 40,000, na kutaka serikali kusema kama huduma hizo ni bure au kuna malipo.

Pia huduma bure kwa watoto nayo ni changamoto kubwa ambayo ni ya muda mrefu nayo imekuwa kilio, na vyote vinachangia kuongeza vifo vya mama na mtoto.

Licha ya jitihada na changamoto nyingi za kibajeti, ni muhimu sana serikali ikatoa kipaumbele cha pekee kuhakikisha dawa zote muhimu zinapatikana hadi ngazi ya zahanati.

Pia hatua madhubuti zichukuliwe kwa wanaoiba dawa, wanaouza dawa kwenye maduka binafsi ambazo zimeshaharibika, kiasi cha kuongeza madhara makubwa ya afya ikiwamo magonjwa yasiyoambukiza.

Kilio hiki ni cha muda mrefu na hasa maeneo ya vijijini, kiasi cha watu ambao hawakustahili kufa wamekufa kwa kuwa tu huduma za afya siyo za kuridhisha na hasa kupata dawa za kutibu magonjwa au kupunguza maumivu.

Lazima serikali kupitia mifumo yake kuziba mianya yote ya upotevu wa dawa, ambayo linagusa na kuumiza wengi na hasa kuzingatia kuwa suala la afya ya mtu siyo la mjadala.

Bila hatua madhubuti, kila bajeti kilio kitajirudia, wananchi wengi wataumia kwa kuwa tu kuna ambao hawakuwajibika. Lazima uwekwe utaratibu sahihi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali kupata dawa sahihi, kwa wakati katoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD).