Kubwa ni kwamba kuna taarifa nyingi zinazotolewa huku zikiwa na upotoshaji mkubwa kuhusiana na chanjo hiyo. Taarifa hizo ambazo hazijathibitishwa na wataalamu wa afya, zinaibua hofu na kusababisha mwitikio mdogo wa watu kwenda kuchanja.
Serikali kwa upande wake imetimiza jukumu lake la kuwalinda raia wake, kwa kutilia mkazo suala zima la umuhimu wa chanjo ya corona, ugonjwa ambao unaendelea kuua watu wengi duniani na wengine kuugua.
Kadhalika, serikali imekuwa ikitoa kauli za kusisitiza usalama wa chanjo hiyo ambayo inatolewa bila malipo.
Kwa kadri takwimu zinavyotolewa, ni dhahiri kwamba mwitikio wa watu kwenda kuchanja hauridhishi kulinganisha na tishio lilivyo, hivyo tunaona kuwa jamii kwa ujumla iwajibike katika suala la chanjo.
Serikali isiachiwe jukumu hilo pekee kwa sababu uhai ni suala la mtu binafsi na sio la serikali. Kwa maneno mengine, wananchi wahamasishane na kuelimishana umuhimu wa chanjo na kwenda kuchanja.
Wanaokataa kuchanja kwa sababu ambazo hazina msingi, ni kikwazo kwa wengine kwa sababu ndio watakaowaambukiza wenzao.
Kadhalika, kuna kikwazo kingine kilichobainishwa kuhusu chanjo, kwamba wanawake wanaonyesha mwitikio mdogo wa kuchanja kulinganisha na wanaume. Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na serikali zilionyesha kuwa wanaume wanajitokeza zaidi kwenye vituo na kuchanja kuliko wanawake, ingawa sababu hazikubainishwa.
Hata hivyo, Mratibu wa chanjo, Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, Boniface Kitikila, amebainisha sababu za wanawake kuwa na mwamko mdogo wa kupata chanjo ya corona.
Alisema kuwa baadhi ya wanaume wanazuia wake zao kwenda kuchanjwa, hali ambayo inasababisha kuwapo kwa wanawake wachache wanaojitokeza kupata huduma hiyo.
Kitikila alisema hayo jijini Dar es Salaam juzi, katika semina ya Jinsia na Maendeleo (GDSS), ambayo ilijikita zaidi kwenye elimu ya kujikinga na UVIKO-19.
Uzoefu wetu unaonyesha kuwa wanawake wamekuwa mstari wa mbele kujitokeza kuliko wanaume katika masuala ya kitaifa kama uchaguzi mkuu, sense na kampeni nyinginezo, hivyo suala la kukatazwa na waume zao nalo linahitaji kutafutiwa ufumbuzi kupitia utoaji wa elimu.
Elimu kwa jamii ndiyo njia pekee ambayo tunaamini kwamba itasaidia kuondoa vikwazo hivi dhidi ya chanjo ya corona.
Tunakubaliana na kauli ya Mkurugenzi Mtendaji wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, aliyoitoa kwenye semina hiyo kwa kuitaka jamii kuepuka kijinsia kwenye chanjo ya corona, ili kila mtu anayehitaji huduma hiyo aipate bila kuzuizi chochote, kwa kuwa ni ya bure.
Tunaamini kuwa kama kuna mwanamume anamzuia mkewe kwenda kupata chanjo ya corona, huo ni ukatili wa kijinsia, ambao haupaswi kuvumiliwa.
Tunaamini kwamba chanjo ndiyo silaha kubwa dhidi ya corona. Mambo mengine kama tiba za asili na kujifukiza ni ya ziada. Tinaikumbusha jamii kuwa corona bado ni janga kubwa.
Baadhi ya nchi kwa kutilia maanani janga hili, zimeamua kuwawekea masharti raia wake ili wachanje, ikiwamo kupata baadhi ya huduma. Tusingependa nchi yetu ifikie huko, hivyo kila mmoja alipe msukumo suala la chanjo ya corona ili kuokoa maisha yake na ya wengine.










