Mpango utoaji mikopo elimu ya juu uboreshwe

12May 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mpango utoaji mikopo elimu ya juu uboreshwe

JUZI Bunge liliagiza serikali kuangalia upya vigezo vya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, ili kupunguza malalamiko ya kutokuwa na vigezo vya ulinganifu yanayojitokeza mara kwa mara miongoni mwa waombaji na wazazi.

Pia liliagiza serikali kuhakikisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inaanza kujiendesha kibenki ili kuwezesha na kurahisisha utoaji na ukusanyaji wa mikopo kwa wanafunzi wanaohitaji mikopo.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Aloyce Kamamba, alitoa ushauri huo wakati akiwasilisha bungeni maoni, ushauri na mapendekezo kwa makadirio ya mapato na matumizi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2022/23.

Alisema serikali iangalie uwezekano wa kuwapatia mikopo wanafunzi wa elimu ya kati pamoja na kuangalia upya vigezo vya utoaji wa mikopo ya elimu ya juu. Alisema hatua hiyo itapunguza malalamiko ya kutokuwa na vigezo vya ulinganifu yanayojitokeza mara kwa mara.

Sambamba na hilo, alishauri serikali kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha ili kuwapatia mikopo wanafunzi wote wanaohitaji mikopo na kwamba ni muhimu bodi ikajiendesha ili kurahisisha utoaji wa mikopo na ukusanyaji wa mikopo kwa wanafunzi wanaohitaji.

Malalamiko ya mikopo yamekuwapo kwa muda mrefu kwamba wanaostahili kupata hawapati, huku wakiwamo ambao wazazi wao wanaweza kuwasomesha lakini wanapewa mikopo.

Wako wanafunzi ambao ni yatima kwa maana ya kwamba hawana baba wala mama, au wametoka kwenye familia maskini lakini wanapoomba mkopo ili waendelee na masomo, wamejikuta wanapata asilimia ndogo huku wenye uwezo wakipata asilimia kubwa.

Wanafunzi wengi wamejikuta wanataabika kwa kuishi maisha magumu, wengine wakishindwa kufanya mtihani kwa sababu hawajalipa ada kiasi cha wadau kuwachangia ili kuendelea na masomo.

Aidha, wazazi wengi husomesha watoto wao kwenye elimu ya msingi na sekondari kwa jasho, wakiamini wakifika chuo kikuu watapata mkopo na itapunguza maumivu, lakini wapo walioshindwa kuendelea na elimu ya juu kwasababu ya kukosa mkopo.

Utoaji wa mikopo umelalamikiwa kwa muda mrefu na watu wengi kwamba hautoi haki sawa kwa wote wanaostahili kupata mikopo, na ndiyo maana wengi wameachwa wakaishi maisha magumu au wengine wakakosa nafasi za kusoma.

Tunaishauri serikali kuliangalia jambo hilo kwa kina, kufanya utafiti wa kina utoaji wa mikopo ili wenye sifa pekee wapate kulingana na matakwa.

Wako waliosomeshwa vizuri na wazazi wao lakini baadaye walifariki dunia au kufilisika wakashindwa kuendelea kusomesha watoto wao, ndiyo maana kumekuwa na kilio cha mikopo kutolewa kwa wote bila ubaguzi.

Wengi wamesema ni muhimu kila mwanafunzi anayeomba mkopo apewe, huku wakienda mbali hadi kwa wenye elimu ya kati ambayo ina wanafunzi wengi.

Pia ni muhimu kuweka mifumo mizuri zaidi ya kurejesha fedha hizo, ikiwamo serikali kuendelea kutengeneza ajira zaidi kwa wanaomaliza vyuo, pia kuwa na mitaala itakayozalisha watu wanaoweza kutengeneza ajira badala ya kutegemea kuajiriwa ambako ni changamoto kubwa kwa sasa.

Inawezekana bodi inaelemewa kwa kuwa fedha zinatoka lakini uwezo wa kurejesha ni mdogo, kwa kuwa wengi wanamaliza vyuo hawana ajira na uwezo wa kurejesha deni hilo ambalo linaongezeka kadri muda unavyosonga.