Mpango wa elimu ya bure umesababisha idadi ya watoto wengi kujitokeza na kuandikishwa kuanza darasa la kwanza kuanzia Januari mwaka huu. Idadi hiyo imepita uwezo wa shule wa kuwahudumia watoto hao na kusababisha changamoto kubwa mbili.
Ya kwanza ni madarasa kutotosheleza idadi ya wanafunzi na ya pili ni shule kuwa na upungufu mkubwa wa madawati. Hali hiyo imesababisha idadi kubwa ya wanafunzi kusomea nje wakiwa wamekaa chini ya miti. Hali hii inazikabili shule zote nchini na kuwaweka walimu katika wakati mgumu kwani ni mazingira ambayo si rafiki katika kutoa elimu.
Ni makosa makubwa kujenga mtazamo kuwa elimu ya bure ni elimu isiyo na ubora. Ubora na viwango bado viko pale pale na si vinginevyo. Jambo la msingi ni kuwa ili kufikia viwango na ubora huo, ni kwa serikali kuwekeza fedha na rasilimali watu (walimu) katika elimu na hilo halihitaji mzaha, bla bla wala porojo.
Maneno bila vitendo yamesababisha tufikie hali tuliyonayo sasa na kuzikwamisha shule za sekondari za kata zisisonge mbele tangu zilipoanza kujengwa mwaka 2007. Kama serikali ingekuwa makini na kuwekeza fedha, leo hii tusingeshuhudia matatizo yanayoendelea kuzikabili shule hizo na kusababisha ufaulu mdogo wa mitihani.
Pamoja na lengo zuri la Rais Dk. John Magufuli, la kutoa elimu ya bure, lakini serikali yake inapaswa kuhakikisha kwamba bajeti kubwa na endelevu inatengwa kila mwaka kwa ajili ya kutekeleza mpango huo.
Tunatiwa moyo na jitihada za Rais Magufuli katika kukabiliana na changamoto zilizojitokeza awali za ukosefu wa madawati na vyumba vya madarasa, kwa kuwaomba mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu wao wakubali kukatwa Sh. milioni moja kwenye mishahara yao ili zipatikane fedha za ujenzi wa madarasa jijini Dar es Salaam na kufikisha Sh. milioni 100 ambazo atazitoa kwa ajili ya kazi hiyo.
Kadhalika, ameahidi kumpatia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadik, Sh. bilioni mbili kuongeza nguvu ya ujenzi wa madarasa sambamba na kuwaeleza wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuwa ambao kwenye maeneo yao kutakuwa na wanafunzi wanaokaa chini watakuwa wameshindwa kazi na hawatakuwa na uhalali wa kuendelea na nafasi zao.
Pamoja na jitihada hizo, sisi tunaamini kuwa sekta ya elimu inahitaji bajeti ya kutosha pengine kuliko sekta nyingine.
Hivyo ni matumaini yetu kwamba changamoto zilizobainika mwanzoni mwa utekelezaji wa mpango wa elimu bure zitaikumbusha serikali kwamba inapaswa kutenga fedha za kutosha katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2016/17.
Taarifa zinaeleza kuwa mwaka huu wanafunzi milioni 1.37 wameandikishwa kuanza darasa la kwanza nchini. Kwa Mkoa wa Dar es salaam pekee kuna wanafunzi 12,000 ambao wamezidi idadi iliyokadiriwa. Ni idadi kubwa inayohitaji serikali kujipanga.
Hivyo basi serikali haina budi kuanzisha mpango maalum kwa ajili hiyo kama serikali ya awamu ya tatu ilivyoanzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MEM) awamu ya kwanza na ya pili. Madarasa mengi yalijengwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Kuanzishwa kwa mpango kama huo sambamba na jitihada za serikali na jamii, kutasaidia kuwa na mipango endelevu ya kutoa elimu bora ya bure na siyo elimu mbovu ya bure.










